Raila aambia Mlima Kenya wamlipe ‘madeni’ yake 2022

Raila aambia Mlima Kenya wamlipe ‘madeni’ yake 2022

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga, amesema analidai eneo la Mlima Kenya ‘madeni’ mawili ya kisiasa linayopaswa kumlipa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga alisema ‘deni’ la kwanza lilitokea mnamo 1963, wakati babake, Jaramogi Oginga Odinga alipokataa kuchukua nafasi ya uwaziri mkuu na badala yake akamuachia Mzee Jomo Kenyatta.

“Babangu Jaramogi alikuwa na nafasi ya kuwa waziri mkuu. Hata hivyo, aliongozwa na uzalendo. Alimwachia Mzee Kenyatta kwani aliamini nchi ilikuwa muhimu kuliko yeye binafsi,” aliambia kituo cha televisheni cha Kameme jana Jumatatu.

Bw Odinga alitaja ‘deni’ la pili kuwa la 2002, wakati Rais Mstaafu Mwai Kibaki alipokiuka mwafaka waliokubaliana naye kuhusu ugavi wa mamlaka baada ya muungano wa Narc kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu mwaka huo.

Akirejelea kumbukumbu kuhusu yale yaliyotokea, Bw Odinga alieleza kuwa kinyume na dhana za wengi, yeye ndiye aliyekosewa.

Aliwalaumu wandani wa Mzee Kibaki kwa kupuuza mwafaka huo: “Tatizo lilitokea wakati wandani waMzee Kibaki walipokataa mwafaka ambao tulikuwa tumekubaliana naye. Wao ndio walileta usaliti wakati akiwa mgonjwa. Walikataa mageuzi ya kikatiba ambayo tulikuwa tumekubaliana. Mimi ndiye nilisalitiwa. Hivyo, Mlima Kenya ndio wako na deni langu.”

Kwa sasa eneo hilo sasa limegawanyika katika mirengo ya kisiasa ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke.’

Mrengo wa ‘Tangatanga’ unajumuisha wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto kwenye azma yake ya kuwania urais mwaka ujao huku ‘Kieleweke’ ikishirikisha wanasiasa wanaounga mkono handisheki na BBI.

Wanasiasa wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakisisitiza haja ya Mlima Kenya kumuunga mkono Dkt Ruto kama njia ya kumlipa ‘deni’ la kusimama na Rais Kenyatta katika chaguzi kuu za 2013 na 2017.

Vile vile, wamekuwa wakirejelea ahadi ya Rais Kenyatta mnamo 2012 kuwa atamuachia Dkt Ruto uongozi baada ya kukamilisha awamu yake ya miaka 10.

Wakati huo huo, Bw Odinga aliwarai wenyeji wa eneo hilo kuunga mkono ripoti ya BBI, akisema ndilo litafaidika zaidi ikiwa itapitishwa.

Aliwaomba kutokubali kupotoshwa na kampeni za “hasla” zinazoendeshwa na Dkt Ruto na wandani wake, akisema zinawarudisha nyuma na kuwanyima watu matumaini maishani.

You can share this post!

Mwigizaji chipukizi shindano la urembo wikendi mtaani...

Ruto apangia UDA mikakati ya chaguzi ndogo