Siasa

Raila aambia Ruto asipoteze wakati ‘meli iling’oa nanga’

September 26th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga amemwambia Naibu Rais William Ruto kwamba anaharibu wakati wake akipinga marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Alisema kwamba yeye na Rais Kenyatta wamejitolea kukamilisha safari ya kurekebisha katiba waliyoanza Machi 2018 walipozika tofauti zao za kisiasa.

“Ripoti ya BBI iko karibu. Wale ambao wamekuwa wakipinga mageuzi kila wakati, wanaotetea makosa na kushamiri katika ufisadi na uongo peupe tayari wamejiandaa kutupinga,” Bw Odinga alisema akihutubia wajumbe wa ODM waliokongamana Nairobi.

Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakipinga BBI wakisema inalenga kubuni nyadhifa za uongozi kunufaisha watu wachache.

Bw Odinga alisema kwamba chama chake kwa ushirikiano na Rais Kenyatta kiko tayari kukabiliana na maadui wa mageuzi.

“Kwa hivyo, ni lazima tujiandae kupigana na maadui wa mageuzi ambao wanataka kusimamisha nchi isisonge mbele,” alisema.

Alisema kwamba wanaopinga BBI ni wale waliopinga demokrasia ya vyama vingi, marekebisho ya Katiba miaka ya 1990s, Katiba Mpya ya 2010, handisheki yake na Rais Kenyatta, wanaopinga vita dhidi ya ufisadi.

“Habari njema ni kuwa tuliwashinda watu hawa wa nia mbaya hapo awali, na ninawaahidi kwamba tutawashinda tena,” alisema.

Dkt Ruto alikuwa mwanachama wa Kanu wakati serikali ya Rais Moi ilipokuwa ikiwakabili waliokuwa wakipigania siasa za vyama vingi. Wakati wa kura ya maamuzi ya 2010 aliungana na viongozi wa makanisa kuipinga. Wakati huu anapinga marekebisho ya katiba ambayo Bw Odinga na Rais Kenyatta wanapendekeza.

Bw Odinga alisema wanaopinga mageuzi ya sasa ni wale wanaonufaika na matunda ya katiba waliyopinga.

Alisema chama cha ODM kinajipanga kuanzia mashinani kote nchini, kuanzisha miungano mipya na vyama vingine na kutia nguvu ushirikiano wake na mrengo wa Rais Kenyatta katika chama cha Jubilee.

“Ni lazima tutie nguvu chama chetu mashinani na kusajili wanachama wapya,” alisema na kusisitiza kuwa kitalenga vijana na wanawake.

Alimshambulia Dkt Ruto na washirika wake akisema wanazua hofu kwa kupotosha raia wakitumia pesa za ufisadi kwa lengo la kuvuruga mageuzi.

“Ni lazima tuwakomeshe wasitumbukize nchi katika ghasia,” akasema.

Kwa kufanya hivi, alieleza, chama chake kinashirikiana na wanasiasa wakongwe waliopigania demokrasia ya vyama vingi na kuwafanya watambue kuwa nchi inahitaji huduma na tajiriba yao wakati huu.

“Tutashauriana na mashirika ya kijamii ambayo hayajapigwa mnada, tushirikiane nayo katika mpango wa People’s Power Project ambao utaanza hivi karibuni,” alisema.

Mpango huu unalenga kukabiliana na kampeni ya Dkt Ruto ya hustler nation ambao ametumia kuvutia idadi kubwa ya vijana.

“Fauka ya yote, ni lazima tupeleke ujumbe kwa watu wetu kwamba mageuzi tunayotaka ni ya kufaidi nchi na kubuni nafasi zaidi kwa kila mtu,” Bw Odinga alisema.

Alisisitiza kuwa marekebisho ya katiba yanalenga kuhakikisha ustawi kwa Wakenya wote, kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi na kuimarisha ugatuzi.