Habari Mseto

Raila aapa kuhakikisha asasi zote zimefanyiwa mageuzi ifikapo 2022

April 22nd, 2018 1 min read

Bw Raila Odinga akihutubu awali. Picha/ Maktaba

Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ameapa kuhakikisha kuwa asasi zote huru za serikali zitafanyiwa marekebisho kabla Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Alisema kwa kurekebisha asasi kama vile Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), taifa litakuwa limepiga hatua ya kwanza kuhakikisha hakutakuwa tena na uchaguzi utakaogawanya Wakenya.

Bw Odinga aliomba mahasimu wake wa kisiasa waungane naye kurudisha umoja wa kitaifa na wakome kuuliza maswali mengi hasa kuhusu ni kwa nini hakushauriana na vinara wenzake wa Muungano wa NASA kabla kutangaza ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Tuna tume nyingi ilhali hazitekelezi wajibu wao jinsi inavyohitajika. Hatuwezi kuwa tunazungumzia 2022 ilhali tungali tunarekebisha matatizo yaliyosababisha usimamizi mbaya wa uchaguzi wa 2017. Hili ndilo jambo tunalotaka kuhakikisha limerekebishwa kabla turudi uchaguzini,” akasema.

Alikuwa akizungumza wakati wa misa katika Kanisa la St Peter’s ACK jana asubuhi, akiandamana na Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o, naibu wake, Dkt Mathew Owili, Bi Ruth Odinga na maseneta maalumu Petronilla Were na Bi Rose Nyamunga.

Alisema salamu yake na Rais Kenyatta ilikomesha uhasama ambao umekuwepo kati ya viongozi wa kisiasa kwa muda mrefu. Alitoa wito kwa wafuasi wake kuunga mkono juhudi za kuleta umoja wa kitaifa huku akipanga kuzindua kamati ya kusimamia juhudi hizo wiki hii.

Bw Odinga amepangiwa kuhudhuria warsha ya ugatuzi Jumatano ambapo atatoa hotuba maalumu katika Kaunti ya Kakamega.

Alisema uhusiano mbaya kati ya magavana na madiwani unafaa kulaumiwa kwa jinsi maendeleo yalivyathirika katika serikali za ugatuzi.

“Inahitajika kuwe na ushirikiano kati ya afisi ya magavana na mabunge ya kaunti. Kile ambacho kimeshuhudiwa katika karibu kila kaunti ni mizozo ya madiwani na maafisa wakuu wa kaunti wakiongozwa na gavana,” akasema.

Bw Odinga alisema hotuba yake itagusia changamoto mbalimbali zinazokumba ugatuzi.