Raila abaki jangwani

Raila abaki jangwani

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, atalazimika kupanga upya mikakati yake ya kuingia Ikulu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, baada ya washirika wake katika muungano wa NASA kumtenga, na chama cha Jubilee kusitisha mchakato wa kuungana na chama chake.

Katika hatua iliyomuacha pweke huku vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais wakiendelea kujipanga, washirika wake katika NASA walitangaza kuwa watajiondoa katika muungano huo kuunda mwingine, One Kenya Alliance (OKA), watakaotumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Odinga alishirikiana na Kalonzo Musyoka wa Wiper ambaye alikuwa mgombea mwenza wake, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula (Ford Kenya) na Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani( CCM) katika muungano wa National Super Alliance (NASA).

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wameungana na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi kuunda OKA, muungano ambao wanasema utaunda serikali ijayo.Mnamo Jumanne, watatu hao walisema kwamba, ili kusuka rasmi muungano wa OKA, vyama vyao vitajiondoa NASA.

“Kuhusu suala la muungano wa NASA, sisi Ford Kenya, Wiper na ANC tunataka kusisitiza kwamba haturudi nyuma katika kujitolea kwetu kufanikisha One Kenya Alliance kwa kushirikiana na Kanu na vyama vingine vilivyo na maono sawa na yetu,” walisema.

“Tunachojua sasa ni kwamba, NASA ni sehemu ya historia yetu,” walisema.Tangazo la vyama hivyo lilijiri siku moja baada ya chama cha Jubilee kusitisha mazungumzo ya kuungana na ODM kikisema kwamba, kilitaka kujipanga kwanza.

“Kwa sasa, tunapanga chama chetu kiwe na nguvu kabla ya kuzungumzia muungano,” alisema naibu katibu mkuu wa Jubilee Joshua Kutuny.Jana, mwenyekiti wa chama cha ODM, John Mbadi, alithibitisha kuwa mazungumzo ya kusuka muungano na Jubilee yamesitishwa.

Hata hivyo, alisema ODM kitaendelea kujipigia debe kivyake kikifanya mikakati ya muungano kitakaoshiriki.“Kwa sasa tunaendelea kuimarisha chama kote nchini tukifikiria kurudi kwa mazungumzo kuhusu muungano,” alisema Bw Mbadi.

Iliibuka kuwa hatua ya chama tawala kusitisha mazungumzo na chama hicho cha chungwa ilitokana na msimamo wa baadhi ya washirika wa Rais Uhuru Kenyatta wanaohisi kwamba Bw Odinga sio maarufu katika ngome ya chama cha Jubilee ya Mlima Kenya.

Bw Odinga alitofautiana na vinara wenzake katika muungano wa NASA baada ya kuwatenga kwenye mazungumzo yake na Rais Uhuru Kenyatta yaliyozaa handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao walinuia kubadilisha katiba kabla ya kuwekwa breki na Mahakama Kuu.

Ingawa hajatangaza kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, vinara wenzake katika NASA wamekuwa wakiapa kwamba hawatamuunga mkono kwenye uchaguzi huo wakisema aliwasaliti.

Vigogo hao wa kisiasa walilaumu Bw Odinga na ODM kwa kukiuka mkataba wa NASA kwa kutogawia vyama tanzu pesa za hazina ya vyama vya kisiasa na kukataa kuunga mmoja wao kwenye uchaguzi mkuu ujao.Chama chake cha ODM kimekuwa kikikashifu viongozi wa vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya kikidai kwamba, NASA haikushinda uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wamekataa wito wa kufufua NASA ili kuwa na nguvu ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2022 hali ambayo wachanganuzi wa siasa wanasema inamuacha Bw Odinga kona mbaya.“Ni kweli taswira iliyopo kwa sasa ni kwamba, Bw Odinga ananing’inia kwa kutengwa na NASA na juhudi za kuungana na Jubilee zikigonga mwamba huku BBI ikipigwa breki.

Nafikiri ni hali ngumu ambayo hajawahi kujipata tangu 2002,” asema mchanganuzi wa siasa Evans Obwaka. Kulingana naye, hiki ni kiuzi ambacho Bw Odinga anaweza kuruka uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa OKA Kanu ikisema haitaacha kuunga Jubilee

Vijana wahimizwa kubuni ajira wenyewe baada ya kupata ujuzi...