Habari MsetoSiasa

Raila adai ufisadi ulimsukuma afunge kiwanda chake

March 5th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amedai ufisadi serikalini na usimamizi mbaya wa mali ya umma ndio uliofilisisha biashara yake Kisumu.

Akizungumza kwa mara ya kwanza jana kuhusu masaibu yanayokumba kiwanda cha utengenezaji bidhaa za sukari guru cha Spectre International, kinachomilikiwa na familia yake, Bw Odinga alikariri msimamo wake kwamba, ni sharti ufisadi uangamizwe kwa manufaa ya wananchi wote.

“Tuna kiwanda cha sukari guru mjini Kisumu. Kiwanda hicho sasa kimefungwa kwa kuwa hakuna sukari guru. Wakati viwanda vya sukari vinapofungwa, hakuna kile tunachoweza kufanya,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika afisi yake iliyo Capitol Hill, Kaunti ya Nairobi baada ya kukutana na Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri walipojadiliana kuhusu mkutano utakaofanywa Kisumu wiki ijayo, kujadili jinsi ya kutatua changamoto za sekta ya sukari .

“Kiwanda hicho kilijengwa Kisumu ili kinufaike kutokana na viwanda vya sukari,” akaendelea kuhusu Spectre, ambacho kilikuwa kikitumia sukari guru kutengeneza kemikali ya ethanol, inayotumiwa katika utengenezaji wa pombe.

Kampuni hiyo imekuwa ikikumbwa na mizozo ya kifedha kati yake na washirika wake kwa miaka kadhaa sasa.

Mnamo 2017, kampuni ya Subira Shipping Contractors ilielekea mahakamani kutaka kiwanda hicho cha familia ya Bw Odinga kifungwe kwa kushindwa kulipa madeni.

Mwezi uliopita, kampuni ya Betric Kenya Limited ilishtaki Spectre International katika Mahakama ya Mombasa ikidai deni la Sh7.7 milioni.

“Tumekubaliana tutakutana na wadau wa sekta ya sukari Jumatatu ijayo mjini Kisumu, kujadiliana kuhusu hatua zitakazochukuliwa ili kubinafsisha sekta hii. Ubinafsishaji utatusaidia tuanze kuleta mashine mpya za kusaga miwa na vilevile pesa, ili shida ambazo zimekumba wakulima kwa miaka mingi zipate suluhisho la kudumu,” akasema.

Serikali ilikuwa imebuni jopokazi maalumu kushauriana na wakulima kuhusu ubinafsishaji wa viwanda vya sukari vikiwemo Muhoroni, SONY, Miwani na Chemelil, ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na hasara kubwa.

Ilibidi vikao visitishwe baada ya baadhi ya wakulima wa miwa kukataa kushiriki mashauriano.