Habari

Raila afahamu kutoa ni moyo – Samson Cherargei

September 12th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Nandi Samson Cherargei amemtaka kiongozi wa ODM Raila Odinga aache kukosoa mpango wa Naibu Rais William Ruto wa kusaidia makundi ya vijana na akina mama kujiimarisha kibiashara.

Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Ijumaa, Septemba 11, 2020, Bw Cherargei alimtaka Bw Odinga kuanza mpango sambamba na wa Dkt Ruto badala ya kutumia muda mwingi kukosoa mpango huo.

“Raila aache kuona wivu kwa ukarimu ambao Naibu Rais Dkt William Ruto ameonyesha kwa vijana na akina mama wanaofanya biashara ndogondogo. Mbona yeye pia asianzishe mpango kama huo wa kutoa misaada ya pikipiki, mikokoteni, vyombo vya saluni na kinyozi, mitambo ya kuosha magari na matangi ya maji?” akauliza.

Bw Cherargei ambaye ni mwandani mkuu wa Dkt Ruto alisema Bw Odinga ni kiongozi anayependa kuendesha “siasa za umaskini” na ndio maana eneobunge alilowakilisha lilibaki nyuma kimaendeleo chini ya uongozi wake kama mbunge kwa miaka 20.

Majuzi Bw Odinga aliuliza ni vipi Dkt Ruto amekuwa akialika makundi ya vijana na akina mama nyumbani kwake Karen, Nairobi na kuwapa misaada ya vyombo mbalimbali ambavyo ni nyenzo kazi.

Juzi katika ziara ya kisiasa katika Kaunti ya Taita Taveta kiongozi huyo wa ODM alisema ni kinaya kwamba Dkt Ruto hutoa misaada hiyo inayogharimu mamilioni ya fedha kuzidi mshahara wake “duni”.

“Tunamuona akitoa mikokoteni, pikipiki na matangi ya maji kwa vijana kufanya biashara. Ni vipi jamaa mmoja anaweza kuchanga zaidi ya Sh100 milioni kwa mwezi mmoja wakati mshahara wake hata haufiki Sh2 milioni? Ni wapi anatoa pesa hizo zote ambazo hata serikali haijui chanzo chake?” Raila aliuliza.

Lakini Bw Cherargei Ijumaa alisema Bw Odinga hajali madhila ambayo huwakumba vijana nchini kwa sababu alizaliwa katika familia tajiri, kwani babake alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza nchini Kenya.

Kwa muda mrefu Dkt Ruto na Bw Odinga wamekuwa wakikwaruzana kuhusiana na mamilioni ya pesa ambazo Dkt Ruto amekuwa akitoa kusaidia miradi mbalimbali ya makanisa na makundi yenye mahitaji maalum.