Habari MsetoSiasa

Raila afufua mjadala wa kura ya maamuzi

August 24th, 2018 2 min read

Na AGGREY OMBOKI

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga, amefufua mdahalo kuhusu kura ya maamuzi kwa kuwaomba Wakenya kujadili Katiba na kuamua iwapo wanafaa kubadilisha baadhi ya vipengele vyake.

Alisema kura ya maamuzi itawapatia Wakenya fursa ya kujadili sehemu za Katiba zinazopaswa kubadilishwa.

Miongoni mwa mambo ambayo anasema yanafaa kuangaziwa wakati wa kufanya marekebisho hayo ya Katiba, ni kupunguza idadi ya wawakilishi, hasa katika ngazi ya kaunti.

Akiongea jijini Nairobi jana, Bw Odinga alisema nchi zingine zina mfumo wa utawala usiokuwa na idadi kubwa ya maafisa.

Alitoa mfano wa Nigeria na Amerika ambazo ingawa zimeendelea kiuchumi, wananchi wake hawana mzigo mkubwa wa wawakilishi.

“Tuko na magavana 47 na manaibu wao pamoja na mabaraza ya mawaziri na mabunge. Mfumo wetu wa utawala unashinda wa Nigeria ambayo ina zaidi ya watu 200 milioni na magavana tisa pekee.

Tunashindana na Amerika iliyo na magavana watano zaidi ya wetu ilhali ina watu wengi na pia ni bara,” alisema Bw Odinga.

Alisema wakati umefika kwa Wakenya kuchunguza katiba iliyopitishwa 2010 kwa lengo la kupendekeza sehemu zinazopaswa kubadilishwa.

“Tunafaa kujiuliza ikiwa tunaweza kumudu mfumo huu na iwapo unafaa kuendelea kuwepo,” aliongeza.

Ilipopitishwa miaka minane iliyopita, Katiba hiyo ilikuwa imepingwa na upande mmoja wa wananchi, lakini ikatoa fursa ya kuifanyia marekebisho baada ya kutumika kwa miaka mitano.

Bw Odinga alisema muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta ulitokana na haja ya Kenya kukabiliana na alichotaja kama vurugu za uchaguzi na migawanyiko ya kikabila kila baada ya miaka mitano.

Alisema kuna wanasiasa ambao hawafurahii mageuzi ambayo yanatekelezwa na serikali kwa wakati huu.

“Kuna watu wanaopinga juhudi hizi ili walinde maslahi yao ya kibinafsi,” alisema Bw Odinga.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema suala la haki katika uchaguzi nchini bado halijatatuliwa akisema baadhi ya watu walipoteza viti vyao baada ya kuibiwa kura.

Kwa mara nyingine, Bw Odinga alisema uamuzi wa kuzungumza na Rais Kenyatta baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa mgumu lakini akaongeza mazungumzo yalistahili ili nchi ipate maridhiano.

“Kuketi na kuzungumza na Uhuru halikuwa jambo rahisi. Lakini Kenya ni kubwa kuliko sisi sote. Sasa tumeanza safari ndefu ya kuunganisha nchi,” alisema.

Alisikitika kwamba Kenya inakumbwa na matatizo mengi ya kiutawala licha ya kuwa na tume kumi na tano zilizobuniwa kuyatatua.

“Tuko na tume nyingi ilhali matatizo zinazopaswa kushughulikia yanaendelea kusumbua Wakenya. Licha ya kuwa na IPOA, mauaji ya kiholela na ukatili wa polisi yanaandama Wakenya,” Bw Odinga alisema.

Alisisitiza kuwa Kenya ina katiba bora, sheria na asasi za kuwezesha katiba kutekelezwa na kuwataka wanasiasa kusaidia kuunganisha nchi.

“Mko katika hali nzuri ya kusaidia raia wa nchi yetu kujiona kama wa nchi moja na kutambua kuwa tabaka au kabila hazitawasaidia wakitenga wengine. Inawezekana kuunda taifa linaloitwa Kenya,” aliwaambia wanasiasa.