Raila ajaribu kumzima Ruto kwa ahadi za vyeo

Raila ajaribu kumzima Ruto kwa ahadi za vyeo

NA WANDERI KAMAU

MWANIAJI urais wa mrengo wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, Jumatatu aligawa serikali yake, kwenye mkakati unaoonekana kukabili muungano wa Kenya Kwanza Alliance (KKA), unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Jumatatu, Bw Odinga alimteua Waziri wa Kilimo, Peter Munya kuendelea kuhudumu katika wizara hiyo, magavana Wycliffe Oparanya (Fedha) na Hassan Joho (Ardhi).

Vile vile, kando na kumteua kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua kama mgombea-mwenza wake, Bw Odinga pia alimteua kuwa Waziri wa Haki na Masuala ya Kikatiba.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hatua ya Bw Odinga inalenga kumkabili kisiasa Dkt Ruto kutokana na baadhi ya ahadi za kisiasa na kiuchumi alizotoa kwa maeneo mbalimbali nchini.

Alipomtangaza mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) kuwa mgombea-mwenza wake Jumapili, Dkt Ruto pia alitangaza makundi tofauti ya viongozi wa mrengo wake ambao watakuwa wakishughulikia masuala ya kiuchumi katika kaunti tofauti.

Dkt Ruto alisema kuwa wamebuni faili ya kila kaunti kuhusu miradi ambayo haijakamilishwa.

“Tumebuni maalum kutoka kila kaunti yatakayotuwasilishia miradi ambayo bado haijakamilika na changamoto zinazowakumba wenyeji. Kwa mkakati huo, itakuwa rahisi kwetu kuitengea fedha na kuhakikisha kuwa utekelezaji wake umekamilika chini ya muda uliowekwa,” akasema Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kumteua Bw Munya kuendelea kuhudumu katika wizara ya kilimo, Bw Odinga analenga kuhakikisha kuwa serikali yake itawafaidi wenyeji wa Mlima Kenya, ambao kitegauchumi chao kikuu ni kilimo.

“Dkt Ruto amekuwa akitoa ahadi nyingi kwa wenyeji wa Mlima Kenya kuhusu juhudi atakazochukua kuboresha bei za mazao muhimu kama kahawa, majanichai, pareto, miraa na sekta ya ufugaji. Sekta hizo ndizo zinategemewa na wenyeji kujiendeleza kimapato. Kwa kumteua Bw Munya, Bw Odinga ameashiria kuwa kinyume na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na mrengo wa Dkt Ruto, hata yeye atakuwa mstari wa mbele kuilainisha sekta hiyo,” asema Bw James Waithaka, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kwa kumteua Bw Oparanya kuwa Waziri wa Fedha, wadadisi wanasema mkakati Bw Odinga kujenga imani kwa wenyeji wa eneo la Magharibi kuwa ameweka mikakati thabiti kuliboresha eneo hilo kiuchumi, hasa kilimo cha miwa.

Kwa upande wake, Dkt Ruto ameahidi kumfanya kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi kuwa Msimamizi Mkuu wa Mawaziri. Kijumla, amewaahidi Bw Mudavadi na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

Hata hivyo, wawili hao wanahitajika kuhakikisha Dkt Ruto amepata uungwaji mkono wa kutosha kutoka eneo hilo.

Wadadisi wanaeleza kwa kinyume na Dkt Ruto ambaye anaonekana kuwaahidi vigogo hao mgao wa serikali, mkakati wa Bw Odinga ni kuonyesha kuwa amempa mmoja wao usimamizi wa wizara ya fedha ili kulainisha kuendesha ufufuzi wa viwanda vya miwa.

Ufasiri uo huo ndio uliopo kwa hatua Bw Odinga kumpa Gavana Joho usimamizi wa Wizara ya Ardhi.

Wadadisi wanaeleza kuwa ikizingatiwa suala la ardhi ni miongoni mwa matatizo ambayo yamekuwa yakilikumba eneo hilo, Bw Joho atakuwa katika nafasi nzuri kuendeleza usuluhishaji wake.

Wanaeleza uteuzi huo unalenga kukabili mpenyo wa Dkt Ruto katika ukanda wa Pwani, ambaye amebuni mkataba wa kisiasa na Gavana Amason Kingi wa Kilifi.

Dkt Ruto ameahidi kumfanya Bw Kingi Spika wa Seneti ikiwa atamwezesha kupata asilimia 50 ya uungwaji mkono katika Kaunti ya Kilifi.

  • Tags

You can share this post!

Karua apaa Kalonzo akifunganya virago

Kalonzo achanganyikiwa baada ya kutoka Azimio, ataka muda...

T L