Raila akanyagia ‘tosha’ ya urithi wa Joho

Raila akanyagia ‘tosha’ ya urithi wa Joho

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, alijiepusha kumwidhinisha mwanasiasa yeyote anayepanga kuwania ugavana Mombasa kupitia chama hicho mwaka ujao alipozuru kaunti hiyo.

Wanasiasa wawili wanaotarajia kushindania tikiti ya chama hicho kuwania ugavana Mombasa mwaka 2022 walionekana kuzidisha juhudi za kutafuta ‘baraka’ za Bw Odinga.

Wawili hao ambao ni Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, walionekana kung’ang’ania sikio la Bw Odinga alipozuru kaunti hiyo Alhamisi.

Bw Nassir na Bw Shahbal hawakukutana ana kwa ana hadharani katika hafla mbili ambazo Bw Odinga alihudhuria akiwa na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho.

Hafla ya kwanza ambayo Bw Odinga alihudhuria ilikuwa ni uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Hass katika mtaa wa Nyali, ambapo Bw Shahbal alikuwepo.

Baada ya kuandamana kwa karibu katika uzinduzi huo, wawili hao walienda kufanya mkutano wa faragha nyumbani kwa Bw Shahbal katika mtaa huo.

Ingawa yale waliyozungumzia hayakuanikwa wazi, duru ziliambia Taifa Leo kwamba, Bw Odinga alimwahidi Bw Shahbal kutakuwa na kura ya mchujo kwa njia ya haki na uwazi kuamua watakaopewa tikiti ya chama kuwania viti vyote vya kisiasa.

Baadaye katika hafla ya kuzindua kitengo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Odinga alikumbwa na miito ya umati uliokuwa ukimtaja Bw Nassir kuwa ‘gavana mtarajiwa’.

Ijapokuwa Bw Joho ndiye alikuwa mwandalizi wa hafla, Bw Nassir ndiye alitembea na waziri huyo mkuu wa zamani sako kwa bako walipowasili katika hafla hiyo. Bw Joho alitembea nyuma yao.

Katika hotuba yake, Bw Odinga alimtambua tu Bw Nassir kama mbunge mahiri ambaye amechangia mengi hasa katika wadhifa wake wa uenyekiti katika kamati ya bunge ya kuchunguza matumizi ya fedha za umma.

“Nataka kutoa shukrani kwa mbunge wa hapa kwa kazi anayofanya kufichua ufisadi katika bunge. Tunataka wabunge wetu waendelee kufanya kazi yao,” akasema Bw Odinga, huku mbunge huyo akisimama kando yake.

Bw Nassir alisema mtu yeyote yuko huru kujiunga na ODM Mombasa lakini ana matumaini makubwa kwamba wapigakura watamchagua yeye kurithi kiti cha Bw Joho.

“Tumeona baadhi ya watu waliokuwa wakikashifu ODM katika uchaguzi uliopita wakirudi kutafuta kiti cha ugavana. Tunawakaribisha kuongezea nguvu chama chetu lakini tunataka wajue mimi ndiye nitakuwa gavana ajaye wa Mombasa. Wapigakura ni werevu, wanajua ni nani anataka kiti hiki kwa manufaa yake ya kibinafsi,” akasema Bw Nassir.

Bw Shahbal alitangaza rasmi kujiunga na ODM kutoka Jubilee wikendi iloyopita. Alikuwa amewania ugavana kupitia Wiper mwaka wa 2013 na Jubilee mwaka wa 2017, lakini Bw Joho akamshinda kwa kuwania kupitia kwa ODM.

Bw Joho alisema angali anatazamia kuwania urais 2022 atakapokamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana ambacho ni cha mwisho kikatiba.

You can share this post!

Walevi Gatundu waasi pombe kujishughulisha na kazi za...

Daktari wa KNH aliyejiua kuzikwa habari zaidi zikiibuka