Habari za Kitaifa

Raila akatiza kampeni za kiti cha AUC ili kutetea madaktari walipwe

April 11th, 2024 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE kiongozi wa upinzani Raila Odinga amevunja kimya chake kuhusu mgomo wa madaktari kwa kuitaka serikali ishughulikie matakwa yao ili warejee kazini.

Waziri huyo mkuu wa zamani Alhamisi Aprili 11, 2024 alisema raia masikini wasioweza kumudu gharama ya huduma za matibabu katika hospitali za kibinafsi ndio wanaumia baada ya mgomo huo kuathiri huduma katika hospitali za umma.

“Hali inaendelea kuwa mbaya na hivi karibuni, huenda tukashuhudia janga kubwa baada wahudumu wote kususia kazi. Tayari maafisa wa kliniki wamejiunga na mgomo huo,” Bw Odinga akasema.

“Kwa hivyo, serikali ikutane na madaktari, wajadiliane kuhusu masuala yaliyoibuliwa ili kukomesha mateso kwa Wakenya,” akaongeza.

Bw Odinga alisema hayo kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi huku mgomo wa madaktari ukiingia wiki yake ya nne.