HabariSiasa

Raila akosa saizi yake

July 17th, 2018 2 min read

VALENTINE OBARA na MOHAMED AHMED

PENGO lililoachwa na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga wakati alipoamua kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, halijapata wa kulijaza miezi mitano baadaye.

Hali hii imeibua wasiwasi katika ulingo wa kisiasa kuhusu hatari ya kuwa na serikali mamlakani bila upande wa upinzani wenye nguvu za kuikosoa kwa ukakamavu inapopoteza mwelekeo.

Waliotarajiwa kujaza pengo la Bw Odinga ni vinara wenza katika Muungano wa NASA ambao ni Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Wengine ni kiongozi wa Thirdway Alliance Ekuru Aukot pamoja na makundi ya kijamii, lakini kufikia sasa hawasikiki na inaonekana upinzani umefifia.

Ingawa kikatiba bunge la taifa ndilo linapaswa kukagua mienendo ya serikali, Bw Odinga ndiye aliyekuwa akitekeleza jukumu hilo hasa kutokana na kuwa idadi kubwa ya wabunge ni wa upande wa Jubilee.

Baada ya kuelewana na rais mnamo Machi 9, alisema anaazimia kubadilisha mtindo wa kutetea mabadiliko ikiwemo kuhusu sheria za uchaguzi kwani mtindo aliokuwa akitumia awali haukuzaa matunda.

Aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, jana alisema ni muhimu pengo hilo lijazwe haraka iwezekanavyo kwani kila taifa la kidemokrasia huhitaji sauti mbadala na ile ya serikali lakini hakuonyesha matumaini ya yeyote mwingine kulijaza isipokuwa Bw Odinga mwenyewe.

“Pengo hilo lisipojazwa Raila atalirejelea. Kwa mtazamo wangu yeye ndiye mwanasiasa shupavu zaidi ambaye nimewahi kushirikiana naye. Nadhani wengine wote ni wanafunzi wake,” akasema Bw Mutunga wakati wa uzinduzi wa kitabu kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2017, kilichoandikwa na mwanahabari John Onyando jijini Nairobi.

Muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta uligawanya Muungano wa NASA na kufikia sasa hatima yake kwani vinara wake wana misimamo tofauti kuuhusu.

Bw Wetang’ula jana alisema mageuzi yaliyokuwa yakipiganiwa na NASA sasa hayana maana tena kwani anaamini Bw Odinga aliwasaliti.

“Hayo yote sasa hayana maana kwa sababu mwenzetu mmoja amepewa nafasi na wale tuliokuwa tunashindana nao, akasahau kuwa Wakenya walikuwa na matumaini kwake,” akasema akiwa Kilifi.

Alijitenga na NASA kufuatia mgogoro uliopelekea kutimuliwa kwake wadhifa wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

Kulingana na Kiongozi wa Chama cha Narc-Kenya, Bi Martha Karua, mageuzi yanayotamaniwa nchini yanaweza kupatikana kama wananchi watashiriki zaidi katika shughuli za vyama vya kisiasa.

“Sote tuna jukumu. Vyama vya kisiasa haviwezi kuwajibika kama wananchi wenyewe hawatavishinikiza. Wengi wetu huwa hawataki kujiunga na vyama vya kisiasa hasa watu wa hadhi ya juu katika jamii,” akasema.

Wito ulitolewa kwa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nchini kujitwika jukumu la kutetea mageuzi nchini.

Kiongozi wa Upinzani nchini Uganda, Dkt Kiza Besigye, ambaye ndiye alikuwa mgeni wa heshima katika uzinduzi huo wa kitabu alisema Kenya imepiga hatua kubwa kidemokrasia barani Afrika lakini ni muhimu kuwe na mijadala wazi kuhusu changamoto zinazokumba taifa na hilo linaweza kutekelezwa na mashirika ya kijamii.

Wakuu wa mashirika ya kijamii wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Haki za Kibinadamu Kenya (KHRC), George Kegoro, walisema hawatarudi nyuma katika majukumu ya kukosoa serikali inapohitajika.