Raila akosoa ushuru wa juu unaotozwa wawekezaji

Raila akosoa ushuru wa juu unaotozwa wawekezaji

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, amekosoa kiwango cha juu cha ushuru kinachotozwa na serikali akisema kinawaumiza wafanyabiashara wa kiwango cha chini.

Bw Odinga alisema kuwa hali hiyo inawatamausha wafanyabiashara hao, ambapo matokeo yake ni kuzorota kwa uchumi wa nchi.

Akizungumza jana, alipohutubu katika Kaunti ya Kiambu, Bw Odinga alisema kiwango hicho kimefanya biashara nyingi kufungwa na watu wengi kupoteza ajira.

Alitoa kauli hiyo alipokutana na wafanyabiashara kutoka ukanda wa Mlima Kenya, katika hali inayofasiriwa kama njia ya kupenya kisiasa katika ukanda huo kwenye matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Alisema kufungwa kwa biashara hizo kumetoa nafasi kwa wafanyabiashara kutoka China kuleta bidhaa kwa ushuru wa kiwango cha chini.

Bw Odinga alisema njia ya pekee ambapo serikali inaweza kubuni mazingira bora kwa ukuaji wa biashara nchini ni kupunguza baadhi ya masharti makali yaliyowekwa. Alieleza hiyo ndiyo njia tu ya kuwapa motisha wafanyabiashara na wawekezaji wanaoanza.

“Mwanzoni, tulikuwa katika kiwango sawa cha maendeleo na nchi kama Singapore, Malaysia na Korea Kusini. Kwa sasa, nchi hizo zimepiga hatua kubwa sana kimaendeleo. Kenya bado inaendelea kubaki nyuma kutokana na ufisadi na maovu mengine ya kijamii,” akasema Bw Odinga.

Aliwarai wafanyabiashara hao kutupilia mbali ukabila na kuungana ili kukuza uchumi wa nchi. Katika siku za hivi karibuni, Bw Odinga amekuwa akifanya vikao na wajumbe mbalimbali kutoka ukanda huo, wadadisi wakisema ni mbinu ya kutafuta uungwaji mkono.

Kwa muda sasa, eneo hilo limekuwa likionekana kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto. Mfanyabiashara Polycarp Igathe, aliyeandaa kikao hicho, alisema umefika wakati kwa Wakenya kukumbatia uongozi unaojikita katika kuimarisha mazingira ya kibiashara nchini.

“Kuanzia mwaka ujao kwenda mbele, lazima tubadilishe mwelekeo na mtazamo wetu. Tumekuwa tukiangazia siasa na wala si masuala ya biashara. Wakati umewadia tubadilishe hayo kwa manufaa ya uchumi wetu,” akasema.

Viongozi walioshiriki katika kikao hicho ni mwanasiasa Peter Kenneth, Kiongozi wa Wachache kwenye Seneti James Orengo, Mbunge Maalum Maina Kamanda, wafanyabiashara Fred Rabong’o, George Wainaina kati ya wengine.

Viongozi hao wamekuwa wakimpigia debe Bw Odinga katika ukanda huo, wakimtaja kama kiongozi atakayehakikisha maslahi yao yamezingatiwa ikiwa atatwaa uongozi.

You can share this post!

Jumwa atangaza kikosi chake 2022

Chama chake Abbiy kifua mbele uchaguzini Ethiopia