Raila alakiwa kishujaa Nyeri akiahidi urafiki wake na jamii ya Mlima Kenya utadumu milele

Raila alakiwa kishujaa Nyeri akiahidi urafiki wake na jamii ya Mlima Kenya utadumu milele

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga Jumamosi anaendeleza kampeni zake kutafuta uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Bw Raila Ijumaa alizuru Kaunti ya Nyeri, ambapo alikutana na baadhi ya viongozi, wazee na vijana. Aidha, kiongozi huyo wa upinzani alionekana kulakiwa kishujaa pamoja na mkewe, Bi Ida Odinga na wazee kutoka Ziwani alioandamana nao. Wazee wa jamii ya Agikuyu, walimvisha mavazi rasmi ishara ya kumkaribisha kuwa miongoni mwao na kumtawaza.

Akiridhia mapokezi hayo, Bw Raila alisema lengo lake ni kuona jamii ya Mlima Kenya na anayotoka Ziwani inaungana na kushirikiana. “Timu niliyoandamana nayo kutoka Ziwani, imekuja kushuhudia wakikaribishwa Mlimani,” Waziri huyo Mkuu wa zamani akasema.

Alikuwa ameandamana na seneta wa Siaya, Bw James Orengo, mbunge mwakilishi wa wanawake Homabay, Bi Gladys Wanga, mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, kati ya wengineo na wazee wa jamii ya Luo.Bi Odinga, vilevile alivishwa mavazi ya kina mama ya jamii ya Agikuyu na kupokezwa kapu lililo na mazao yanayozalishwa eneo la Mlima Kenya, naye akirejesha mkono kwa kapu lenye samaki.

Nyanza inafahamika katika ufugaji na uvuvi wa samaki, Mlima Kenya ikiwa mzalishaji mkuu wa viazi, mboga na matunda, na pia mazao mengine yanayochukua muda mfupi kuzalisha. “Tutashirikiana, tuboreshe urafiki wetu udumu milele na milele,” Raila akaahidi.

Kiongozi wa ODM alitumia jukwaa la ziara hiyo kuuza sera zake kuwania urais mwaka ujao. Alitaja sekta ya kilimo, viwanda na uongezaji thamani kama baadhi ajenda ambazo atatilia maanani zaidi ili kuboresha maisha ya wakazi wa eneo la Kati. “Tutaweza kubuni nafasi za kazi kwa vijana wetu na pia nkupiga jeki kina mama. Na ndio maana ninasema tuuungane na kushirikiana,” akaelezea.

Bw Raila amekuwa akishirikiana na serikali tawala ya Jubilee, hasa baada ya maafikiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, Machi 2018, maarufu kama Handisheki. Wawili kupitia salamu za maridhiano, walitangaza kuzika katika kaburi la sahau tofauti zao za kisiasa na kuahidi kusaidiana kuunganisha taifa.

Ni ushirikiano ambao umesababisha Rais Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto ‘kutengana’, licha ya wawili hao kushirikiana kwa karibu 2013 – 2017 walipochaguliwa.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Vigogo wa kisiasa wasitumie kesi ICC...

Ruto: Rais hatakuwa ameafikia ajenda zake atakapostaafu

T L