Raila alegeza kasi ya maandamano kuenda Ikulu

Raila alegeza kasi ya maandamano kuenda Ikulu

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa Azimio Raila Odinga ameashiria kulegeza kamba kuhusu mpango wa maandamano mnamo Jumatatu.

Awali, Bw Raila alikuwa ametangaza kwamba wafuasi wa muungano wa Azimio wataandamana kuelekea Ikulu wakitaka matakwa kadha wa kadha yatimizwe na serikali ya Rais William Ruto.

Waziri Mkuu huyo wa zamani siku ya Jumamosi, hata hivyo, aliashiria kulegeza misimamo mikali aliyoweka.

Huku Ikulu jijini Nairobi ikiwa makao ya Rais yenye ulinzi mkali, Raila alisema Azimio itatuma wawakilishi kuwasilisha malalamishi yao.

“Kama atakuwa Ikulu, tutatuma watu sio umati. Tutatuma wajumbe,” Bw Raila alisema.

Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga. PICHA | MAKTABA

Kulingana na kiongozi huyo wa chama cha ODM, msafara wa maandamano utatangulia Afisi ya Rais Harambee House, katika kitovu cha jiji la Nairobi.

“Endapo hatakuwa humo, watakaochaguliwa tutawatuma Ikulu wamkabidhi rasmi malalamishi yetu au wayaweke langoni,” Raila alielezea.

Alisema wajumbe watakaotumwa watateuliwa na kwamba hajui iwapo atakuwa mmoja wao.

“Sijui ikiwa nitaenda, ila nikichaguliwa ni sawa. Wanachama wa Azimio ndio wataamua.”

Aliorodhesha matakwa ya upinzani kwa serikali ya Kenya Kwanza, yanayojumuisha; kushusha gharama ya maisha mara moja, sava ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufunguliwa ili kujua aliyeshinda urais Agosti 9, 2022 na kukomesha uundaji wa tume nyingine ya uchaguzi akisema makamishna waliojiuzulu na kufutwa wanapaswa kurejeshwa kazini.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, mahakama ya upeo ilifutilia mbali kesi ya Raila kuhusu utata wa matokeo ya urais na kuidhinisha ushindi wa Dkt Ruto.

“Endapo alichaguliwa kwa njia halali baada ya kukagua sava ya IEBC, tutamtambua kama rais,” Raila akasema.

Serikali imeonya upinzani kuhusu maandamano yatakayozua vurugu.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Asema kuelewa mahitaji ya mteja ndio siri ya...

ICC yatoa agizo Putin akamatwe kwa uhalifu

T L