HabariSiasa

Raila alifika JKIA akiwa mlevi chakari – Miguna Miguna

May 21st, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MWANAHARAKATI wa upinzani Miguna Miguna ameanzisha vita vya maneno dhidi ya mlezi wake kisiasa Raila Odinga, kwa kumtelekeza wakati alihitaji usaidizi wake hali iliyochangia kufurushwa kutoka nchini.

Dkt Miguna pia alimkejeli Bw Odinga kwa kujifanya kuwa mzalendo ilhali ni dikteta mkubwa.

“Anaongea kana kwamba alizuiliwa pamoja nami ilhali alifika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) akiwa mlevi chakari. Alishindwa kuongea… isitoshe hangesimama kwa miguu yake miwili,” akaongeza.

Bw Odinga hakujibu madai hayo, kutokana na ushauri kutoka kwa mkurugenzi wake mawasiliano wa chama cha ODM Philip Etale.

Bw Etale alimshauri kutomjibu Bw Miguna “kwa sababu sio mtu wa tabaka lako, kisiasa.”

Bw Miguna alisema Wakenya wengi ambao waliunga mkono mageuzi katika mfumo wa uchaguzi na haki bado wanauliza ni kwa nini aliachana na kampeni za mageuzi na kuungana na serikali.

“Maridhiano ambayo Raila anatetea akiwa pamoja na Uhuru Kenyatta inakwenda kinyume cha kampeni za kutetea haki katika uchaguzi, haki ya kijamii, heshima kwa katiba na uhuru wa idara ya mahakama,” akaongeza.

Kulingana na Bi Miguna, mpango wa Raila wa kujenga madaraja kwa ushirikiano na Serikali ya Jubilee hauwezi kusuluhisha changamoto zinazoikabili taifa hili.

“Hatuwaogopi Raila na Kenyatta…. tutakabiliana na hulka ya kudharau sheria bila woga wowote,” akasema.

“Huu mpango wa maridhiano utafeli kwa sababu ni njama ya watu wawili kuwahadaa Wakenya ili wasahau makosa ambayo waliwafanyia. Hawa sio viongozi wenye maoni na Wakenya wenye nia njema wanafaa kuwakataa,” akafoka.

Shambulio la Miguna dhidi ya Raila lilijiri saa chache baada ya kiongozi huyo wa upinzani kudai kuwa masaibu yaliyompata mwanaharakati huyo yalitokana na hali kwamba alikataa kushirikiana na maafisa wa Idara ya Uhamiaji katika JKIA.

Bw Odinga alisema hayo Jumamosi alipotoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza.