Raila alilia vijana Nyanza wajisajili kwa kura za 2022

Raila alilia vijana Nyanza wajisajili kwa kura za 2022

Na WAANDISHI WETU

KINARA wa ODM, Raila Odinga jana alirejea nyumbani kuwalilia vijana katika eneo la Nyanza kujisajili kuwa wapigakura ili kumwezesha kupata ushindi katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao wa 2022.

Bw Odinga alisema kujikokota kwa vijana wa Nyanza kujisajili kuwa wapigakura ni mfano mbovu kwa watu wa maeneo mengineyo ambao wamejitolea kuunga mkono azma yake ya kuwania urais mwaka ujao.

Bw Odinga aliagiza viongozi wa Nyanza kuanzisha kampeni kali za kuhamasisha watu kujisajili kuwa wapigakura.Kiongozi huyo wa ODM alikuwa ameandamana na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, wabunge Roza Buyu (Kisumu), John Mbadi (Suna Kusini), Fred Ouda (Kisumu ya Kati), Spika wa Kisumu Elisha Oraro kati ya viongozi wengineo.

“Nimetembea kote nchini lakini kila mahali ninaenda wananisukuma kuwania urais. Lakini ninahofia ngome yangu – wamekataa kujisajili kuwa wapigakura. Hatuwezi kwenda vitani ilhali maaskari wangu hawana vitambulisho vya kitaifa kama bunduki na kadi ya wapigakura ambayo ni sawa na risasi,” akasema Bw Odinga.

Kaunti za Nyanza ni kati ya maeneo ambayo yameshuhudia idadi ya juu ya wapigakura wapya ambao wamejitokeza kujisajili ili kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 mwaka ujao.Shughuli ya kuwasajili wapigakura wapya kwa wingi inatarajiwa kukamilika wiki ijayo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inalenga kusajili wapigakura wapya 727,661 katika eneo la Nyanza. Lakini kufikia sasa ni wapigakura wapya 71,208, sawa na asilimia 9.7, pekee ambao wamejisajili.

Baadhi ya maeneo ya Mlima Kenya kama vile Kiambu, Nyeri, Nyandarua na Murang’a pia yameshuhudia idadi ya chini ya waliojitokeza kujisajili kuwa wapigakura.Bw Odinga jana alihutubu katika maeneo ya Ahero, Rabuor, Nyamasaria, Kondele na Kituo cha Mabasi cha Kisumu katika juhudi za kushawishi vijana kwenda kujisajili kuwa wapigakura.

Bw Odinga alisema kuwa serikali yake itatoa kipaumbele kwa masilahi ya vijana endapo atachaguliwa kuwa rais mwaka ujao.Alisema serikali yake itaendeleza mpango wa Kazi Mtaani nao vijana wanaoanzisha biashara hawatatozwa ushuru.

Gavana Oparanya aliwataka wakazi wa Nyanza kujisajili kupiga kura huku akisema eneo la Magharibi litamuunga Bw Odinga katika kivumbi cha urais.Huku Bw Odinga akiwarai wakazi wa Nyanza kujisajili, Naibu wa Rais William Ruto jana alikita kambi katika eneo la Ukambani ambapo aliwarai wakazi kuachana na kiongozi huyo wa ODM katika uchaguzi mkuu ujao.

Hiyo ilikuwa mara ya pili mwezi huu kwa Naibu wa Rais kuzuru eneo la Ukambani kujipigia debe.Aliwataka wakazi wa eneo hilo kujiunga na cahama chake cha United Democratic Alliance (UDA).

Dkt Ruto alisema kuwa Bw Odinga hajafanyia lolote eneo la Ukambani licha ya kumpigia kura kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa 2013 na 2017.Dkt Ruto alizuru eneo hilo huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka – ambaye ni kinara wa kisiasa wa eneo hilo – akishinikizwa kuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Gavana wa Kitui, Charity Ngilu na kundi la wazee kutoka eneo la Ukambani wameonya kuwa huenda Bw Musyoka akajipata katika baridi ya kisiasa iwapo atashikilia msimamo wake wa kuwania urais 2022.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Raila akiacha dhana ya ‘mradi’ ishike...

Shahbal atetea mradi wa nyumba Buxton

F M