Habari MsetoSiasa

Raila alipotoshwa kuungana na Uhuru – Mashirika

April 1st, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MASHIRIKA ya kijamii yamemtahadharisha kiongozi wa NASA Raila Odinga kwamba muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta huenda ulinuiwa kumvuta kuunga utawala wa Jubilee ili kuvutia uwekezaji na ufadhili wa kigeni.

Kwenye taarifa, mashirika hayo yalisema matukio ya hivi punde yameonyesha kuwa huenda Bw Odinga alipotoshwa kuhusu manufaa ya muafaka huo.

“Iwapo muafaka unahusu utawala wa sheria, ilikuwaje waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i, Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet na Katibu wa Uhamiaji Gordon Kihalangwa walipuuza maagizo ya Mahakama na kumfurusha Miguna Miguna hadi Dubai bila Rais kusema lolote,” ilihoji taarifa iliyotiwa saini na mshirikishi wa muungano wa mashirika hayo (CSRG), Suba Churchill.

“Hali hii inaweza kumaanisha kitu kimoja tu, kwamba ni serikali iliyopanga hayo na haiwezi kujitakasa kutokana na lawama za umma na aibu iliyopata kimataifa,” alieleza Bw Churchill.

Alisema kinyume na Bw Odinga alivyofanywa kuamini kwamba akishirikiana na serikali angelinda sifa zake, ni wazi kuwa serikali ya Jubilee inamtumia kiongozi huyo wa upinzani ili kuvutia ufadhili, huku ikiendeleza utawala mbaya, wizi, ukiukaji wa haki za binadamu na haki za kimsingi bila kujali.

“Mashirika ya kijamii hayataunga mwafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga iwapo hautazingatia haki za binadamu,” ilisema taarifa ya mashirika hayo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa matukio yaliyofuatia kurejea nchini kwa Bw Miguna Miguna kulikotibuliwa yanathibitisha kuwa serikali haiwezi kutekeleza makubaliano kati ya Rais na Bw Odinga.

“Kwa hivyo, CSRG inamtahadharisha Raila kuwa mwangalifu na asisite k mwafaka huo iwapo serikali ya Jubilee itaendelea na njama yake ya kupuuza utawala wa sheria,” mashirika hayo yanamuonya Bw Odinga.

Bw Churchill alisema kuwa Rais Kenyatta alishindwa kutumia fursa ya wazi ya kurejea nchini kwa Miguna kudhihirisha kwamba alikuwa na nia ya dhati ya maridhiano kisiasa ya kuunganisha nchi.

“Ikiwa yaliyompata Miguna katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na anaendelea kutesekea katika uwanja wa ndege ugenini ni kwa sababu ya kumwapisha Raila Odinga kama Rais wa Wananchi, basi ni wazi kuwa Rais Kenyatta hakuafikiana na waziri huyo mkuu wa zamani kwa moyo wake wote,” alisema Bw Churchill.

Alisema matukio hayo yanaonyesha kwamba Rais Kenyatta angali na kinyongo moyoni na itakuwa vigumu kutekeleza aliyokubaliana na Bw Odinga.

Alisema kupigwa kwa wanahabari waliokuwa wakifuatilia kurejea nchini kwa Bw Miguna na maafisa wa polisi ni onyo kwa Raila kwamba hafai kuunga mkono serikali inayotumia ghasia na nguvu dhidi ya raia wake.