Makala

MUTUA: Raila alisaliti Wakenya alipomezwa na serikali

July 4th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KILA nikiwaza kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais wa marudio nchini Malawi ninamkasirikia kinara wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga.

Raila, ambaye anapaswa kuwa kiongozi wa upinzani nchini Kenya ila yumo serikalini katikati, alihalalisha haramu aliposusia uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26, 2017, ulioagizwa na Mahakama ya Juu.

Uchaguzi wa Malawi ulifanyika hivi majuzi kwa maagizo ya mahakama baada ya kugundulika kwamba Rais Peter Mutharika aliiba kura katika uchaguzi wa Mei 2019.

Aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa Malawi wakati huo, Bw Lazarus Chakwera, alifanya kampeni kabambe, akashiriki uchaguzi huo na kumbwaga Mutharika! Sasa Chakwera ndiye Rais wa Malawi, naye Mutharika ni Rais mshinde.

Raha iliyoje kujua kwamba ushindi wa Chakwera ulifanikishwa na ushirikiano wa vyama kadhaa vya upinzani, ambavyo vilimuunga mkono! Kumbe hata Afrika watu wakijitahidi wanaweza kumshinda Rais wasiyempenda?

Hatua ya Chakwera kushiriki uchaguzi huo wa marudio ni kinyume na alivyofanya kigogo wa siasa za upinzani nchini Kenya.

Bw Odinga aliwaamuru wafuasi wake wasusie uchaguzi wa marudio wa 2017, eti kwa sababu masharti fulani aliyotoa hayakutimizwa, amri iliyomwezesha Rais Uhuru Kenyatta kuwa kwenye debe bila mshindani huyo stadi.

MARUDIO YA UCHAGUZI MALAWI

Nina hakika Bw Odinga alipoona mambo yalivyokwenda Malawi aliyakumbuka matukio ya mwishoni mwa 2017 kwa majuto makubwa.

Bila shaka sasa Bw Odinga ni msiri mkuu wa Rais Kenyatta, sikwambii amepata hata mgao wa bajeti hali cheo chake rasmi hatukijui, lakini lazima kimoyomoyo anajiambia ‘labda ningeshiriki uchaguzi huo ningekuwa rais sasa hivi’.

Akitoa masharti ya kushiriki uchaguzi huo, Bw Odinga alisema yasingalitimizwa angaliususia kwa kuwa hali ilivyokuwa ilimpendelea mpinzani wake wa wakati huo, Rais Kenyatta.

Hapo ndipo alipojikosea na akatukosea sote Wakenya kwa sababu alimpa Rais Kenyatta fursa ya kuzidisha shinikizo dhidi yake ili Bw Odinga asiwanie.

Nimesema Bw Odinga alitukosea kwa sababu hatua yake hiyo iliashiria kwamba Rais Kenyatta ndiye mkuu wa kila kitu nchini Kenya, vitendo vyake havingepingika kamwe. Muonjeshe fisi kipande cha nyama atakuvaa mzimamzima na kukutafuna!

Usisahau uchaguzi huo wa marudio ulikuwa umeagizwa na mahakama ya Kenya, si Uropa wala Marekani kunakojulikana kwa idara za mahakama huru kabisa.

Nakumbuka vizuri sana Jaji Mkuu David Maraga, akiufutilia mbali uchaguzi wa Agosti 2017 na kuagiza mwingine urudiwe kuambatana na sheria lau sivyo huo nao aufute pia. Ujasiri ulioje!

KUKOSA BUSARA

Hivyo basi, ukizingatia kwamba tayari Bw Odinga alikuwa amemshinda Bw Kenyatta mahakamani, na kuhakikishiwa akitendwa tena arejee huko huko, utakubaliana nami kwamba uamuzi wa kuususia haukuwa wa busara.

Mahakama ya Bw Maraga ilikuwa tayari ishampata mwizi wa kura na kumwaibisha kimataifa, lakini bado Bw Odinga alikuwa na shaka nayo.

Kwa kuususia, Bw Odinga alimpa fursa Bw Kenyatta, chama cha Jubilee na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujitakasa uchafu waliopata kwa kukoroga uchaguzi wa Agosti 2017.

KUSHIRIKIANA NA ALIYEMHINI

Kana kwamba hilo halikuwa chungu zaidi, Bw Odinga alitia msumari moto kwenye donda la wafuasi wake kwa kushirikiana na aliyemhini na kunufaika na wizi wa kura za Agosti.

Hapo ndipo haramu ilipoharamishwa kabisa; mauaji yaliyohusishwa na uchaguzi wa Agosti kama vile ya Bw Chris Msando pamoja na ya mamia ya wafuasi wa NASA yakawa si hoja.

Laiti Bw Odinga angalijua kwamba si lazima awe Rais, bora haki itendeke. Kupita njia ya mkato kwa manufaa yake binafsi, japo wapo wanaouita huo utaifa, ni usaliti dhidi ya wafuasi wake na nafsi yake mwenyewe ambao utaishi kumkwaza daima.

Chakwera wa Malawi angekutana na Mutharika faraghani wapokezane mikono asingalikuwa Rais leo hii. Subira huvuta heri.

 

[email protected]