HabariSiasa

Raila alivyoingiza Uhuru mtegoni

July 15th, 2019 2 min read

JUSTUS OCHIENG Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga alitumia vitisho vya kujitenga kwa maeneo yaliyokuwa yakimuunga mkono kwenye uchaguzi wa 2017 katika kumsukuma Rais Uhuru Kenyatta kuingia handisheki, imeibuka.

Kulingana na Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju, ambaye pia sasa ni mshauri wa Bw Odinga, Rais Kenyatta hakuwa na budi ila kukubali muafaka kwa ajili ya kudumisha taifa moja.

Bw Tuju alisema kuwa handisheki ndiyo iliyokuwa suluhisho pekee kwa mjadala wa kujitenga kutoka Kenya.

“Kabla ya handisheki kuna baadhi ya watu waliokuwa wamezua mjadala wa kujitenga. Kwa hivyo unajiuliza ni nani angetaka kuongoza nchi ambayo idadi kubwa ya watu wanaotaka kujitenga?” akasema Bw Tuju kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Bw Odinga alinukuliwa wakati huo akisema waliokuwa wakitoa mwito huo walikuwa na sababu nzuri kutokana na kile alichokitaja kama “ubaguzi wa kikabila tangu uhuru”.

Mjadala huo ulikoma ghafla Machi 9, 2018 wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga walipoafikia handisheki.

Suala la kujitenga kwa maeneo ya upinzani lilizuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 wafuasi wa Bw Odinga walipodai ushindi wao uliibwa.

Bw Tuju alisema hatima ya Kenya ilitegemea utatuzi wa masuala ya kushirikisha wote kwenye serikali ili kila mmoja ajihisi ni raia kamili wa nchi hii.

“Wale wanaopinga juhudi za kuwaunganisha Wakenya wanaharibu mshikamano wa jamii ya Kenya. Nani angetaka kuongoza taifa lililotengana?” akasema Bw Tuju.

Bw Tuju alieleza kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa na kipindi kigumu kuamua kuafikiana kutokana na wandani wao waliokuwa na misimamo mikali.

Alisema nchi ilikuwa inapitia kipindi kigumu sana na iliwabidi Rais Kenyatta na Bw Odinga kuchukua uamuzi ulioweka taifa mbele ya masuala mengine.

Wakati huo huo, vita vya maneno vimeibuka ndani ya Jubilee baada ya kubainika kuwa Bw Tuju anafanyia kazi ODM akiwa mshauri wa kisiasa wa Bw Odinga.

‘Usaliti’

Naibu Rais William Ruto Jumapili alimshutumu Bw Tuju kwa usaliti. “Yaani demokrasia yetu imekua kiasi kwamba Katibu Mkuu wa chama tawala anageuka kuwa mshauri wa Upinzani! Maajabu,” akasema Dkt Ruto kupitia mtandao wa Twitter.

Naye Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria alisema Jubilee kilikufa Rais Kenyatta alipotangaza kushirikiana na Bw Odinga.

“Rafiki yangu Dkt Ruto. Chama cha Jubilee kilifariki Machi 9, 2018. Raphael Tuju ni mjumbe tu. Usishambulie mjumbe aliyetumwa,” Bw Kuria akamwambia Bw Ruto.

Chama cha ODM, hata hivyo, kilipuuzilia mbali madai kwamba Bw Tuju ni mshauri wa Bw Odinga: “Chama cha ODM kina washauri wa kutosha na hakihitaji watu kutoka nje kutushauri,” akasema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Philip Etale.

Hii ni mara ya pili kwa Bw Tuju kushambuliwa na kundi la ‘Tangatanga’ linalounga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Mwezi uliopita, wanasiasa wa kundi hilo walitaka Bw Tuju atimuliwe kwa kuzua mgawanyiko baada ya mazungumzo ya simu baina yake na mwanasiasa wa Kiambu George Nyanja kuchipuza mtandaoni.

Wanasiasa hao pia wamekuwa wakimtaka Rais kuitisha mkutano wa Jubilee.