Habari za Kitaifa

Raila alivyojiundia ikulu ndogo wiki moja baada ya washirika kuteuliwa serikalini


AFISI ya kiongozi wa ODM Raila Odinga iliyoko Capitol Hill Square, imegeuka kuwa ikulu ndogo ya aina yake huku ikitembelewa na watu mashuhuri wakiwemo maafisa wa serikali, wiki moja baada ya washirika wake kuteuliwa mawaziri.

Sawa na ilivyokuwa alipozika tofauti zake na Rais Uhuru Kenyatta 2018, Bw Odinga amekuwa akipokea watu mashuhuri baada ya ukuruba wake wa kisiasa na Rais William Ruto.

Jana, alitembelewa na Katibu wa Wizara ya Fedha Chris Kiptoo katika Capitol Hill, jambo ambalo lilikuwa mwiko kabla ya ukuruba wake na Rais Ruto.

Picha zake na Bw Kiptoo zilisambazwa mtandaoni na kuashiria mwamko mpya kati yake na serikali. Isitoshe, naibu wa balozi wa Kenya Ujerumani Valerie Rugene pia alimtembelea afisini mwake.

“Waziri wa Fedha Chris Kiptoo alinitembelea katika Capitol Hill Square. Tulijadili masuala makuu yanayoathiri uchumi,” Bw Odinga alichapisha katika mitandao yake ya kijamii jana.

Taifa Leo imefahamu kuwa, Bw Odinga, baada ya washirika wake kuteuliwa Mawaziri, anaweza pia kutengewa nafasi kadhaa za makatibu na tayari washirika wake wameanza kung’ang’ania nyadhifa hizo.

Mbali na Capitol Hill Square, nyumbani kwake Karen kumekuwa na shughuli nyingi kuliko kawaida huku watu wakijipanga na hali yake mpya.

Raila akiwa na Valerie Rugene ambaye ni Naibu Balozi wa Ujerumani, katika afisi yake Nairobi. Picha|Hisani

Wasaidizi wake walitueleza kwamba, yanayoendelea ofisini na nyumbani kwake ni sawa na alipokuwa Waziri Mkuu.

Bw Odinga anashikilia kuwa hayumo serikalini. Hata wakati wa Handisheki 2018 hadi 2022, alisisitiza hakuwa sehemu ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta. Hata hivyo, yanayoshuhudiwa ni tofauti. Kupitia yanayonaswa kwenye kamera ndani ya ofisi yake, ni wazi kuwa ana ushawishi mkubwa.

Huku kukiwa na mzozo kati ya Dkt Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua, inachukuliwa kwamba mtu yeyote sasa yuko salama zaidi anapoonekana kujitambulisha na Bw Odinga.

Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba ikiwa Ikulu ni jengo lililo Mlimani, basi Capitol Hill ndio njia ya kuekelea Ikulu, ikiwa sio ikulu mbadala.

Ni kisa cha historia kujirudia. Baadhi ya picha za Bw Odinga akiwa ndani ya Capitol Hill wakati wa handisheki ni pamoja na akiwa na Alfred Mutua (Julai 2019), Mike Sonko (Aprili 2018), Anne Waiguru (Desemba 2019), Joshua Kutuny na Zedekiah Kiprop (Septemba 2020), Peter Munya na Anyang’ Nyong’o (Agosti 2019), Charity Ngilu (Aprili 2019), Alex Tolgos (Agosti 2020), Nancy Macharia (Januari 2019), Robert Godec (Juni 2018), Joe Nyagah (Novemba 2018), Hassan Joho na Amason Kingi (Machi 2019), miongoni mwa wengine.

Kutokana na maoni yaliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii, Capitol Hill Square inaweza pia kuwa mashine ya kutakasa walio na doa, ambapo watu wanaoandamwa na ufisadi hujitokeza na ghafla wanaacha kukashifiwa na upinzani.

Maoni ya Wakenya kwenye X, kwa picha ya Bw Odinga akitangaza ziara ya Dkt Kiptoo yanaonyesha jinsi Wakenya wanavyochukulia ziara kama hizo.

“Sanitaiza!” aliandika Cornelius Ronoh.

Kelvin Kiptoo aliuliza: “Je, serikali ya upinzani au upinzani uko serikalini?”

“Maafisa wa serikali sasa wanaripoti Capitol Hill kwa kushauriwa na Raila kuhusu jinsi ya kusimamia uchumi,” aliandika Mallo Fredrick.