Habari MsetoSiasa

Raila amechangia pakubwa kwa umaskini magharibi mwa nchi – Echesa

July 15th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA Waziri wa Michezo Rashid Echesa sasa amemlaumu kiongozi wachama cha ODM Raila Odinga, kuwa ndiye sababu eneo la Magharibi limekuwa nyuma kimaendeleo, kwa kumuunga mkono miaka yote.

Bw Echesa alimkashifu Bw Odinga kuwa amekuwa akitumia wakazi wa magharibi kujinufaisha kisiasa, kwa kuwaomba kura kila uchaguzi, lakini baadaye wanaposhindwa anawatelekeza.

Aliendelea kusema kuwa sababu ya viwanda vilivyovuma eneo hilo miaka ya mbeleni kufa ni kutokana na hali kuwa wamekuwa wakishikana na watu ambao hawashindi chaguzi.

“Tumechoka kucheza pata potea na maisha ya watu wetu, tumemuunga mkono kwa muda mrefu bila kupata kitu,” akasema.

Alisema japo jiji la Kisumu limekuwa likipata maendeleo na kupata wawekezaji, mji wa Kakamega haujakuzwa kwa njia sawia, hali aliyosema inaonyesha jinsi wametelekezwa.

“Kuna tofauti kubwa kati ya Kisumu na Kakamega kimaendeleo. Raila hajatuletea maendeleo hapa. Kisumu kuna uwanja wa ndege na wawekezaji hujaa huko kwa sababu hiyo,” akasema Bw Echesa, ambaye alitimuliwa kutoka kiti chake cha uwaziri miezi kadha iliyopita.

“Tumemuunga mkono hii miaka yote lakini amemtupa mmoja wetu (Mudavadi),” akasema mwanasiasa huyo.

Aidha, alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kumtafutia kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi kazi, akisema ni Rais aliyewatafutia Bw Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.