HabariSiasa

Raila amfokea Matiang'i kwa kudai majaji ni wakora

April 4th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa Upinzani Raila Odinga Jumatano amemkemea Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kwa kudunisha Idara ya Mahakama.

Bw Odinga alisema matamshi yaliyotolewa na Dkt Matiang’i ambapo alitaja baadhi ya majaji katika Idara ya Mahakama kuwa ‘walaghai, wakora na waovu’, ni ya kiholela.

“Wiki nne zilizopita mimi na Rais Uhuru Kenyatta tuliafikiana kushirikiana katika kuleta amani ,” akasema Bw Odinga kupitia taarifa yake aliyotuma katika vyombo vya habari.

“Lakini nilikerwa mno kuona Waziri wa Usalama Fred Matiang’i akishambulia na kuwadhalilisha baadhi ya majaji wa mahakama kwa kutumia lugha ya kijeuri.  Matamshi hayo hayafai  kutolewa na afisa wa serikali,” akaongezea.

Bw Odinga alisema matamshi hayo ya Dkt Matiang’i ni sumu kwa mwafaka baina yake na Rais Kenyatta ambapo waliafikiana kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi mnamo Machi 9, 2018.

Bw Odinga aliwataka wabunge kukoma kutumia vikao vya kamati mbalimbali kuwa majukwaa ambapo maafisa wa serikali wanashambulia na kudunisha Idara ya Mahakama.

“Tumekuwa na kipindi kirefu cha sarakasi za kisiasa na sasa kila kiongozi ana jukumu la kuhakikisha kuwa tunakuwa na amani kwa kuepuka kutoa matamshi yanayogawanya nchi,” akasema Bw Odinga.