HabariSiasa

Raila ampiku Ruto Ikulu

May 16th, 2019 2 min read

 
Na LEONARD ONYANGO
 
USHAWISHI wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga serikalini unaendelea kuongezeka huku wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi uliopita wakitumia afisi yake kuomba kazi kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni kinyume na kabla ya handisheki mwaka 2018, ambapo waliotaka kazi walikuwa wakitumia zaidi ushawishi wa Naibu Rais William Ruto.

“Wakati wa muhula wa kwanza wa Jubilee, Dkt Ruto alionekana kuwa na ushawishi mkubwa serikalini kiasi kwamba wawekezaji na hata wanasiasa wengine walionekana kuanzia kwake kabla ya kumfikia Rais.

“Lakini sasa mambo yanaonekana tofauti na wanaelekea katika afisi ya Bw Odinga. Hiyo ni ishara kwamba amejipatia ushawishi mkubwa,” anasema wakili Felix Otieno.

Kulingana na mshirika wa karibu wa Bw Odinga, wengi wa wanasiasa wanaoomba kazi za serikali kupitia kwa waziri huyo mkuu wa zamani ni wa chama cha Jubilee kutoka Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

“Wanasiasa wengi wamekuwa wakija Capitol Hill kukutana na Bw Odinga tangu handisheki. Wengi huwa wanaleta stakabadhi zao wakiomba awasaidie kufikisha maombi yao ya kazi kwa Rais Kenyatta,” akasema mmoja wa wandani wa Bw Odinga.

“Wengi wao hutafuta kazi za ubalozi na katika bodi za mashirika mbalimbali ya umma,” akaongeza.

Wanasiasa ambao walinufaika kutokana na uteuzi wa majuzi uliofanywa na Rais Kenyatta ni pamoja na Dennis Waweru, Nicholas Gumbo, Frankline Bett, Kembi Gitura, Kabando wa Kabando na Ochieng Mbeo.

Wengine ni Jamleck Kamau, Shakila Abdala, Stephen Ngare na Julius Malombe.

Mbali na wanasiasa wanaosaka kazi, mawaziri pia ni miongoni mwa wakuu serikalini ambao wamekuwa wakitafuta uhusiano wa karibu na Bw Odinga kutokana na kuwa anasikizwa zaidi na Rais Kenyatta.

Mnamo Jumatatu wiki hii aliandamana na mawaziri watatu, Peter Munya (Biashara), James Macharia (Uchukuzi) na John Munyes (Madini) katika ziara ya kuzindua miradi mbalimbali Kaunti ya Kisumu.

Ushawishi wa Bw Odinga pia umejitokeza kwa kutambuliwa kwake na mabalozi na viongozi wa mataifa ya kigeni. Mwezi uliopita, balozi wa Amerika Kyle McCarter alikutana naye katika jumba la Capitol Hill, siku moja baada ya kutembelewa na balozi wa Ethiopia humu nchini Meles Alem.

Aliyekuwa balozi wa Afrika Kusini humu nchini Koleka Mqulwana, mwezi uliopita alifika afisini Capitol Hill kumuaga Bw Odinga kabla ya kurejea nyumbani baada ya muda wake kukamilika.

Bw Odinga ndiye pia alimsindikiza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi alipohudhuria kongamano la One Planet lililofanyika Machi mwaka huu jijini Nairobi.

Kiongozi huyo pia amekuwa akipokea jumbe kutoka maeneo mbalimbali ya nchini. Mnamo Aprili 8, alitembelewa na viongozi kutoka jamii ya Wakalenjin wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat.
Bw Salat aliteuliwa na Rais Kenyatta kuwa mwenyekiti wa Posta mwezi mmoja baada ya kikao hicho na Bw Odinga.

Rais Kenyatta amekiri mara mbili kuwa Bw Odinga yuko serikalini na amekuwa akishauriana naye kabla ya kufanya maamuzi yenye umuhimu kwa taifa.

Rais Kenyatta amekuwa akisema wamekuwa wakizungumza kwa sauti moja na Bw Odinga katika masuala ya kukabiliana na ufisadi na kufanyia mabadiliko Katiba.