Michezo

Raila amtaka Wanyama asaidie kukuza vipaji nchini

June 19th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KIUNGO mkabaji wa Tottenham Hot Spurs Victor Wanyama ametakiwa asaidie kuimarisha viwango vya soka hapa nchini kwa kuwakuza na kuwalea wachezaji chipukizi.

Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga alimtaka kiungo huyo wa timu ya taifa Harambee Stars atekeleze majukumu hayo wakati Wanyama alipomtembelea katika ofisi yake ya kibinafsi ya Capitol Hill jijini Nairobi Jumanne mchana.

Bw Odinga ambaye ni shabiki mkubwa soka ni mdhamini mkuu wa Klabu ya Gor Mahia  na katika mechi zinazoendelea za Kombe la Dunia anashabikia bingwa mtetezi Ujeramani ambao waliona vimulimuli kwa kulishwa kichapo cha 1-0 kwenye mechi ya kwanza waliyocheza dhidi ya Mexico Jumapili usiku.

“Victor Wanyama wa Tottenham Hot Spurs alinitembelea. Nilimtaka aimarishe kiwango cha soka nchini kwa kuwakuza vijana chipukizi wenye talanta ili waweze kufikia kiwango alichofika na hata zaidi,” akasema  Bw Odinga.

Wanyama yupo likizoni baada ya msimu wa mwaka 2017/18 ya ligi kuu nchini Uingereza EPL  kukamilika ambapo klabu yake ilimaliza wa tatu nyuma ya Mabingwa Man City na nambari mbili Manchester United kwenye msimamo wa jedwali la ligi hiyo.

Jumapili, Wanyama alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliotazama mchuano wa kirafi wa soka ulioandaliwa na mchezaji mwenzake katika kikosi cha timu ya taifa na mshambulizi wa Girona FC ya Uhispania Michael Olunga.

Wanyama ndiye mkenya wa kwanza kucheza katika ligi ya Uingereza baada ya kusakatia awali Klabu za Celtic nchini Scotland kisha akajiunga na Southhampton kabla ya kutua Tottenham Hot Spurs.

Mwanadimba huyo anatarajiwa kurejea mjini London Julai 7 kushiriki mechi za kirafiki za kabla ya msimu na klabu yake ambayo ni ya pekee kutoka jiji la London iliyofuzu kushiriki ligi ya klabu bingwa barani Uropa msimu 2018/19.