Raila amtetea Ruto

Raila amtetea Ruto

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga amewataka wabunge kutupilia mbali mswada unaolenga kuharamisha matumizi ya kaulimbiu ya ‘Hasla’ inayotumiwa na Naibu Rais William Ruto katika mikutano yake ya kampeni.

Bw Odinga alisema kuwa Naibu Rais pamoja na wandani wake hawafai kuzuiliwa kutumia kaulimbiu hiyo ambayo inahofiwa na baadhi ya viongozi kwamba huenda ikazua vita baina ya Wakenya maskini na mabwanyenye.

Katika juhudi za kuzima kampeni za Dkt Ruto zinazotoa taswira ya ulinganisho baina ya watu wa mapato ya chini na matajiri, kuna wabunge wanaopendekeza mswada unaopiga marufuku kauli hiyo katika mikutano ya kisiasa.

Wabunge wanapendekeza kiongozi anayepatikana na hatia ya kusababisha chuki za matabaka ya kiuchumi aondolewe ofisini.

Ikiwa mswada huo utapitishwa kuwa sheria, itakuwa pigo kwa kampeni ambazo Dkt Ruto amekuwa akitumia kupigia debe azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Ruto na wandani wake wamejipachika nembo ya mahasla wakidai kwamba matajiri wanataka kukwamilia mamlakani.

Amekuwa akiandaa mikutano kote nchini kuendeleza kampeni hiyo akitaja handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kama muungano wa matajiri wanaotaka kubadilisha katiba kuwanyima watu wa mapato ya chini nafasi ya kuongoza.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, wamekosoa kampeni hiyo wakisema inalenga kusababisha vita vya matabaka. Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa familia yake na ya Rais Kenyatta zilitoka katika usuli wa kimaskini.

Mswada huo uliopendekezwa na Kamati ya Usalama ya Bunge chini ya uwenyekiti wa mbunge wa Kiambaa, Bw Paul Koinange, unapendekeza faini ya Sh5 milioni kwa wanaopatikana na hatia ya kugawanya Wakenya kwa misingi ya matabaka.

Kwenye mkutano na kamati ya usalama ya bunge mapema mwaka huu, Mwenyekiti wa NCIC, Bw Samuel Kobia alisema kampeni ya mahasla dhidi ya matajiri inaweza kutumbukiza nchi katika ghasia.

Alisema kampeni hiyo ni hatari nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Alipohutubia viongozi wa eneo la Mlima Kenya mwanzoni mwa mwezi huu, Rais Kenyatta pia alisema kampeni hizo zinawagawanya Wakenya kwa misingi ya matabaka.

Jumatano, waziri mkuu wa zamani, Bw Raila, alipomtetea Dkt Ruto kupitia mtandao wa kijamii, alisema hivi:

“Nimefahamishwa kwamba kuna mswada ambao unalenga kupiga marufuku kaulimbiu ya ‘mahasla’ yake Naibu wa Rais Ruto. Mswada huo unapendekeza adhabu kali kwa watakaopatikana wakitumia kauli hiyo.

“Hali sawa na hiyo ilitokea mnamo 1933 na 1945 nchini Ujerumani ambapo kiongozi wa nchi Adolf Hitler alichochea mauaji ya halaiki kwa misingi ya matabaka ya kiuchumi, rangi na kabila.” Kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa japo anahofia kuwa matumizi ya kaulimbiu ya ‘mahasla’ huenda ikasababisha fujo nchini, Dkt Ruto pamoja na wandani wake hawafai kuzuiliwa kwani wana haki ya kujieleza.

“Badala yake, japo sisi tunaohofia kwamba huenda kauli hiyo ikazua machafuko nchini, tuna jukumu la kuelimisha Wakenya waiepuke ili wasijehadaiwa. Nina imani Wakenya watajua ukweli na kujitenga na udanganyifu huo,” akasema Bw Odinga.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet , Bw Kipchumba Murkomen, hata hivyo, jana walipuuzilia mbali madai kwamba wanagawanya Wakenya.

“Sisi hatujawahi kugonganisha maskini dhidi ya matajiri. Tumekuwa tukihimiza kwamba maskini (mahasla) wawezeshwe kujiinua kimapato,” akasema Seneta Murkomen.

Dkt Ruto amekuwa akijiita hasla huku akisema kuwa aliishi maisha ya umaskini ambapo aliuza kuku katika eneo la Turbo, Uasin Gishu kabla ya kuwa bwanyenye.

Wabunge wengine wanaoegemea upande wa Dkt Ruto walisema msimamo wao ni kutetea vijana ambao wengi wao huteseka kwa kukosa ajira.

Leonard Onyango, Benson Matheka na Onyango K’Onyango

You can share this post!

Bandari na Ingwe kupigania pointi KPL Ijumaa

Huenda wandani wa Ruto Kisii wakamtoroka hivi karibuni