Raila amtumia Ruto ujumbe wa muungano

Raila amtumia Ruto ujumbe wa muungano

PATRICK LANG’AT na JUSTUS OCHIENG’

DALILI zimeibuka kwamba muungano kati ya Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga unasukwa kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Hii ni baada ya Dkt Ruto kukutana na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ambaye ni mwandani Bw Odinga na pia Naibu Mwenyekiti wa chama cha ODM.

Dkt Ruto alikutana na Bw Oparanya akiwa ameandamana na mawaziri wa zamani Mwangi Kiunjuri na Rashid Echesa katika hoteli ya kifahari ya Mahali Mazuri iliyoko katika mbuga ya Maasai Mara, Kaunti ya Narok mnamo Jumatano mchana na hapo jana.

Mkutano huo umeibua msisimko kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga, ambao wamekuwa mahasimu wakubwa kisiasa tangu 2010, hatimaye wameridhiana na wapo tayari kushirikiana ili kutwaa uongozi wa nchi 2022.

Duru kutoka hoteli hiyo ziliarifu Taifa Leo kwamba, viongozi hao wawili waliwasili kwa ndege tofauti saa tano mchana na wakarejea tena Alhamisi.

Hapo jana Bw Oparanya alithibitisha kufanyika kwa mkutano huo, na kuupuza umuhimu wake japo akakiri kwamba ODM na UDA inayohusishwa na Dkt Ruto, ziko tayari kufanya kazi pamoja siku zijazo.

“Ulikuwa mkutano wa kibahati tu wala haukupangwa. Kwa kuwa mimi ni mwanasiasa, naibu rais aliuliza iwapo tunaweza kufanya kazi pamoja. Hata hivyo, nilimwaambia uamuzi kuhusu suala hilo unaweza kutolewa na chama baada ya majadiliano kulihusu,” akasema Bw Oparanya.

Hata hivyo, alikataa kufichua mengi huku matamshi yake mengi yakiashiria kuwa kuna majadiliano yanayoendelea kati ya ODM na UDA.

Bw Echesa na mwenyeji wao mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo pia walikanusha kuwa mkutano huo ulipangwa na ulilenga kujenga muungano kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto.

“Hizo ni propaganda za mitandaoni kwani tulikuwa na mkutano wetu kisha Bw Oparanya akawa pia hotelini humo, akaja akatusalimia kisha akaondoka,” akasema Bw Echesa.

“Wachana na hilo tukio. Kila moja wetu alikuwa na masuala ya kushughulikia kisha tukaondoka,” akasema Bw Tongoya.

Wiki mbili zilizopita, Dkt Ruto alimiminia Bw Odinga sifa kama kiongozi ambaye amejenga chama kinachowaunganisha Wakenya, akionekana kuungana naye kuwakemea viongozi wa One Kenya Alliance (OKA) ambao wamemtenga waziri huyo mkuu wa zamani kisiasa.

OKA inajumuisha kinara wa ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya ambao walimuunga mkono Bw Odinga 2017 chini ya Nasa.

Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi pia yupo kwenye muungano huo.

Aidha, kakake mkubwa Bw Odinga, Dkt Oburu Oginga hivi majuzi alinukuliwa akisema kuwa muungano kati ya nduguye na naibu rais haufai kupuuzwa baada ya kubainika kuwa viongozi wa OKA wana baraka za Rais Kenyatta.

Dkt Ruto na Bw Odinga waliungana pamoja mnamo 2005 na kuunda chama cha ODM kisha wakafanya kazi pamoja katika serikali ya muungano.

Baadaye walitengana na kila moja kwenda njia yake kisiasa. Kiini cha kufarakana kwao wakati wa utawala wa Jubilee ni muafaka kati ya Rais na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018.

Wandani wa Dkt Ruto na wale wa Bw Odinga nao wameonekana kuchangamkia muungano kati ya wanasiasa hao wawili wakuu nchini, wakisema hakuna jambo linalowazuia kushirikiana licha ya uhasama ambao umekuwa kati yao kwa zaidi ya miaka 10.

You can share this post!

Kenya sasa yaanza kujitengenezea silaha

MCK yalaani mauaji katili ya mwanahabari wa KBC