HabariSiasa

Raila anadi upatanisho kwa jamii ya Waluo

April 24th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, ameomba wazee wa jamii ya Waluo wazidi kuendelea kupatanisha jamii hiyo na zingine nchini.

Akizungumza Jumatatu baada ya kukutana na wazee hao katika boma lake la Opoda lililo Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema wazee hao sasa wamekubali kushirikiana baada ya kuwa na mizozo ya uongozi kwa muda mrefu.

Mkutano huo ni wa karibuni zaidi kati ya Bw Odinga na viongozi wenye ushawishi kwa jamii katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono kwa mikakati anayoendeleza ya kupatanisha taifa baada ya kutangaza ushirikiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita.

Alisema walikubaliana Mzee Willis Otondi aendelee kuwa mwenyekiti wao huku Bw Nyandiko Ongadi akichaguliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu.

“Katika siku za hivi majuzi kumekuwa na mivutano ambayo imetishia kugawanya baraza la wazee. mkutano wa leo umeleta umoja na wazee wamekubali watakuwa wakishirikiana kwa uongozi wa Mzee Otondi,” akasema Bw Odinga.

Aliongeza: “Watakuwa wakishauriana na wazee wa jamii zingine nchini. Tuna imani ya kwamba kuanzia leo wazee watakuwa wanafanya kazi vile inavyotakikana.”

Mbali na kupatanisha jamii hiyo na zingine nchini, baraza hilo pia litaendeleza jukumu lake la kutunza mila na desturi za kijamii kwa kudumisha tamaduni muhimu na kuhimiza zilizo hatari zitupiliwe mbali.

Bw Otondi aliahidi kudumisha umoja wa baraza hilo ambalo mizozo yake iliyohatarisha kugawanya jamii imewahi kupelekwa mahakamani wakati mmoja.

“Kutoka sasa tutaendelea kwa umoja. Kazi yetu kama mnavyojua ni kuunganisha Waluo na vile vile kujaribu kuleta wazee wa maeneo mengine pamoja,” akasema.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, ambaye alisema alihudhuria kama wakili ili maelewano yaliyofanywa na wazee yaidhinishwe kisheria.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Bw Odinga kukutana na baraza hilo la wazee tangu alipotangaza ushirikiano wake na Rais Kenyatta.

Ushirikiano wa kinara huyo wa upinzani na serikali uliibua hisia tofauti miongoni mwa jamii ya Waluo ambao ndio wafuasi wake wakuu zaidi wa kisiasa.

Baadhi yao walihisi kusalitiwa baada ya kujitolea mhanga kumtetea wakati aliposema aliibiwa kura baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Wiki iliyopita, Bw Odinga pia alikutana na wabunge wa zamani wa maeneo ya Luo Nyanza katika afisi yake iliyo Capitol Hill, jijini Nairobi.