Habari

Raila anarudi siku chache zijazo kupigia debe BBI – Joho

June 27th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga tayari amefanyiwa upasuaji na anatarajiwa kurejea nchini siku chache zijazo.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho mnamo Ijumaa aliwahakikishia Wakenya kuwa Bw Odinga sasa ni buheri wa afya baada ya kufanyiwa upasuaji mgongoni.

Bw Odinga aliondoka humu nchini Jumapili kuelekea Dubai, Milki za Uarabuni (UAE) ambapo amekuwa akitibiwa katika hospitali moja ya Kijerumani, kulingana na ndugu yake, Dkt Oburu Odinga.

Dkt Oburu ambaye ni mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Jumatano alisema kuwa Bw Odinga alikuwa anafanyiwa upasuaji ‘mdogo’ mgongoni wala hapakuwa na shaka wala chochote cha kuwatia wafuasi wake hofu.

Dkt Oburu alisema nchi ya Ujerumani inamiliki hospitali inayotoa huduma za matibabu ya kiwango cha juu jijini Dubai ambapo ndugu yake anatibiwa.

Duru za kuaminika kutoka katika familia ya Bw Odinga ziliambia Taifa Leo kuwa waziri huyo mkuu wa zamani alifanyiwa upasuaji Jumanne.

Ijumaa, Bw Joho alisema aliridhishwa na hali ya Bw Odinga baada ya kuzungumza naye kwa simu.

“Nimepata fursa ya kuzungumza na kiongozi wa chama na ‘baba yangu’. Ninajihisi mwenye furaha kwamba anaendelea vyema. Sisi kama wanachama wa ODM tunaendelea kumwombea Baba (Raila),” akasema Bw Joho kupitia video aliyochapisha katika mitandao ya Twitter na Facebook.

Bw Joho alisema kuwa kiongozi huyo atarejea humu nchini kuendeleza Mpango wa Maridhiano (BBI).

Jopokazi la BBI linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kufikia Jumanne, Juni 30.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa ripoti hiyo itacheleweshwa ili kusubiri Bw Odinga kurejea humu nchini kabla ya kuiwasilisha.

“Nina hakika kwamba Baba atarudi humu nchini hivi karibuni na kuendelea na ajenda yake ya kuunganisha Wakenya. Tunaunga mkono ajenda yake; maono yake ndiyo tunayofuata,” akasema Bw Joho.

Naibu huyo wa kiongozi wa ODM pia aliwataka Wakenya kuwaombea viongozi wao kwani wao pia wanapitia changamoto mbalimbali, ikiwemo kuwa wagonjwa.

“Tukumbuke kwamba hata viongozi wetu ni binadamu na wanaweza kuwa wagonjwa na wanapitia changamoto mbalimbali sawa na watu wengine. Tunapoomba tuwaombee viongozi wetu,” akasema Bw Joho.

Kabla ya Dkt Oburu Odinga kujitokeza wazi na kusema kuwa kiongozi wa ODM anatibiwa Dubai, mitandao ya kijamii ilisheheni madai kwamba alisafirishwa kisiri hadi China kwa ajili ya matibabu ya dharura.

Dkt Oburu alisema Bw Odinga hangeweza kupelekwa katika taifa hilo la bara Asia kwa kuhofia kuwekwa karantini ya lazima kwa siku 14 chini ya uangalizi wa kijeshi.

Uvumi ulipoenea wikendi kuhusu hali ya afya ya Bw Odinga, chama cha ODM kilidai kuwa alielekea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).