Habari MsetoSiasa

Raila angali yafiki yangu – Namwamba

February 24th, 2019 1 min read

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Msaidizi wa Mashauri ya Kigeni Ababu Namwamba amezika tofauti baina yake na bosi wake wa zamani katika chama cha ODM, Raila Odinga.

Akiongea katika kipindi cha mjadala katika runinga moja ya humu nchini, mbunge huyo wa zamani wa Budalang’i alisema hana chuki zozote na kiongozi huyo wa ODM licha ya kutofautiana naye kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.

“Raila angali rafiki yangu hadi wakati huu. Tungali tunazungumza kila mara licha ya kwamba miegemeo yetu ya kisiasa ni tofauti,” Bw Namwamba akasema.

Waziri huyo msaidizi pia alipongeza muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga akisema umeleta utulivu mkubwa katika ulingo wa kisasa.

“Utulivu huu unaotokana na handisheki kati ya wawili hao umeimarisha mazingira ya uwekezaji humu nchini na utendakazi wa serikali kwa ujumla,” Bw Namwamba akasema.

“Inafurahisha kwamba tumeungana kwa mara nyingine chini ya Rais Kenyatta. Ipo haja kwa sisi kama viongozi kuelekeza juhudi zetu sasa katika mchakato wa kupalilia maridhiano na kuzika siasa za migawanyiko kwenye kaburi la sahau,” akaeleza.

Bw Namwamba ambaye zamani alikuwa Katibu Mkuu wa ODM alijijenga kisiasa kwa kujinadi kama mfuasi sugu wa Bw Odinga.

Lakini wanasiasa hawa wawili walikosana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 kwa sababu ya utata kuhusu uchaguzi wa ODM. Hali hiyo ilichangia Bw Namwamba kugura ODM na kujiunga na chama cha Labour Party of Kenya (LPK).