Habari Mseto

Raila angeshinda angejenga nyumba kwa hivyo sijui kwa nini mna shida mimi kuzijenga

February 5th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto, Jumapili alieleza kufurahia hatua ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kutambua mpango wa serikali wa kujenga nyumba za bei nafuu, akisema hilo linafaa kumaliza majibizano ambayo yamekuwepo kuhusu mpango huo.

Akihutubu kwenye ibada moja ya kanisa katika Kaunti ya Kakamega, Rais Ruto alisema mpango huo ulikuwa kwenye manifesto za mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja, hivyo hakupaswi kuwa na pingamizi zozote zinazofaa kuwa zikitolewa kuuhusu.

“Ikiwa Azimio ingebuni serikali, wangeutekeleza kwa njia yao. Hata hivyo, ikizingatiwa sisi (Kenya Kwanza) ndio tulio uongozini, tunautekeleza kwa njia yetu. Kila mmoja anafaa kuelewa hivyo, ili kutuwezesha kuendesha mpango huu mzuri utakaotoa nafasi za ajira kwa vijana wetu katika fani za uhandisi, useremala, uashi, utengenezaji bidhaa, uchimbaji mawe, uchoraji ramani za nyumba, uchukuzi kati ya nyingine,” akasema.

Mnamo Jumamosi, Bw Odinga alisema kuwa mpango huo hauna makosa yoyote, japo akakosoa utaratibu ambao serikali inatumia kuutekeleza.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, akisema kuwa ndiye aliyekuwa mwanzilishi wa mpango huo.

Alisema alibuni mpango huo alipohudumu kama Waziri wa Barabara na Ujenzi, kwenye serikali ya Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki.

Alisema kuwa alizuru mataifa kama Malaysia, Singapore na Hong Kong, kufahamu jinsi mpango wa nyumba za bei nafuu huwa unaendeshwa na kuwafaidi raa wa mataifa hayo.

Alieleza alifanya ziara hizo hata kabla ya serikali ya Narc kuanza mpango huo na uboreshaji wa mitaa ya mabanda.

“Mpango niliokuwa nao pamoja na Bw Kibaki si wa kuwalazimisha watu kulipa ada ili baadaye kununua nyumba hizo. Ni wa kuwapa uhuru watu kufanya maamuzi kuhusu ikiwa wangetaka kununua nyumba hizo au la,” akasema Bw Odinga.

Serikali imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi kutekeleza mpango huo, baada ya mahakama kutoa maamuzi kadhaa kusimamisha utekelezaji wake.

Hata hivyo, serikali imeapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa kusimamisha utekelezaji wake.