Habari za Kitaifa

Raila aogopa ‘salamu’ za Gen Z, abadili msimamo kuhusu handisheki na Ruto

Na JUSTUS OCHIENG July 11th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga Jumatano alipiga abautani kuhusu uwezekano wa serikali ya muungano huku chama chake cha ODM kikiunga mazungumzo ya kitaifa yanayopangwa kuanza wiki ijayo.

Bw Odinga alikosolewa vikali na vijana mtandaoni kufuatia ripoti kwamba, Rais William Ruto anawazia kuunda serikali ya muungano kushirikisha baadhi ya viongozi wa upinzani.

Wakati wa kutiwa saini mswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) mnamo Jumanne, Bw Odinga aliunga kauli ya Rais William Ruto kuwa, suluhu kwa mzozo ambao taifa linalopitia kwa sasa ni mazungumzo.

Kauli hiyo ilimweka pabaya miongoni mwa vijana hao ambao walimshambulia mitandaoni wakimtaja kama mwanasiasa msaliti ambaye ameungana na serikali kuwapiga vita na kutatiza juhudi zao za ukombozi.

Baadhi hata waliandika barua iliyosambaa mitandaoni ikionya Umoja wa Afrika (AU) dhidi ya kumruhusu waziri huyo mkuu wa zamani awanie kiti cha uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AUC). Bw Odinga analenga wadhifa huo ambao uchaguzi wake utafanyika Februari mwaka ujao.

Wengine nao walitoa picha za zamani na kumdhihaki Bw Odinga kwa kila aina ya neno mitandaoni.

Walidai alikuwa amehongwa na utawala wa Kenya Kwanza ili kumpunguzia Rais shinikizo ambazo zilikuwa zikimkabili kisiasa.

Kati ya waliotofautiana na Raila ni mwanawe Raila Jnr ambaye alisema msimamo wa babake haufai kufasiriwa kuwa wake eti kwa sababu tu wao ni somo.

Jana, ODM, chama anachokiongoza Bw Odinga kilipinga mazungumzo hayo na kumwaambia kinara huyo wa upinzani kuwa Wakenya wengi hawana nia ya kushiriki shughuli hiyo kwa kuwa wanaipinga.

“Nimeambiwa na hawa viongozi kwamba, mmesema hamtaki salamu za maridhiano. Ujumbe umefika,” akaandika Bw Odinga katika ukurasa wake wa X baada ya kukutana na baadhi ya viongozi wa ODM akiwemo Katibu Mkuu wa Chama Edwin Sifuna.

Kulikuwa na ripoti kuwa Rais Ruto alikuwa akiwazia kubuni serikali ya muungano ambapo wanasiasa wa upinzani wangetunukiwa nyadhifa serikalini.

Gen Z wamekuwa wakipigania mageuzi makubwa ndani ya utawala wa sasa wakiwakashifu viongozi serikalini kwa kuhusika na ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka. Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuwatuliza iwapo yatafanyika.

Jana, Raila alionekana kujihadhari baada ya onyo la Gen Z waliomponda na kufasiri uungwaji mkono wake kwa mazungumzo kama usaliti.

Kabla ya Bw Odinga kubadilisha msimamo, Mwenyekiti wa ODM John Mbadi, alikuwa ametuma taarifa iliyosema chama kilikuwa kikiunga mkono mazungumzo hayo.

“Si siri kuwa kwa sasa taifa lipo katika njia panda na lazima mmoja wetu aonyeshe uzalendo nchi isonge mbele,” ikasema taarifa iliyokuwa imetumwa na Bw Mbadi.

Mbunge huyo Maalumu alikuwa amesisitiza kuwa ODM ni chama ambacho kinaamini katika mazungumzo ili kusuluhisha masuala ambayo yanazua utata.

“Kiongozi wa chama ameongea na nimekuwa na nafasi ya kukutana naye na kuzungumzia suala hili. Sisi sote tuna makubaliano kuwa ana nia njema kwa nchi ndiposa anasema masuala yanayoibuka yasuluhishwe kupitia mazungumzo,” akaongeza Bw Mbadi.

Bw Mbadi pia aliwaendea wale ambao walikuwa wakimshambulia Raila mitandaoni, akisema kiongozi huyo anafahamu vyema jinsi anavyopanga mikakati yake ya kisiasa.

“Mtu hafai kutuzomea kuhusu maandamano. Tumekuwa hapo awali na sisi tunafuata tu amri ya baba wala hatujawahi kuogopa kupambania raia na nchi,” akasema Bw Mbadi.

Kutokana na mkengeuko wa Raila wengi wanasubiri kuona iwapo mazungumzo hayo yataendelea na kufanikiwa kwa kuwa vijana wameapa kuyasusia.