Raila apinga matokeo ya IEBC

Raila apinga matokeo ya IEBC

NA SAMMY WAWERU
 
MGOMBEA wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga amepinga matokeo yaliyotangazwa Jumatatu na Tume Uhuru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
 
Bw Raila ametaja Jumanne matokeo yaliyotolewa na mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati kama “batili na tupu”.
 
“Tunapinga vikali matokeo ya urais yaliyotangazwa jana Jumatatu na Bw Chebukati,” waziri huyo mkuu wa zamani amesema, akihutubu KICC, Nairobi.
 
Raila amezungumza kwa mara ya kwanza tangu matokeo yaliyotangazwa rasmi kuonyesha naibu rais, William Ruto (Kenya Kwanza) anaongoza katika kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu ulioandaliwa mnamo Agosti 9, 2022, ambapo alizoa kura 7,176, 141, sawa na asilimia 50.49.
 
Kinara wa Azimio alipata kura 6,942,930 (asilimia 48.85), kiwango ambacho kilimuorodhesha mgombea wa pili.
 
“Tutatumia njia zote Kikatiba na kisheria kutafuta haki,” Bw Odinga akasema.
 
Jumatatu, muda mfupi kabla Chebukati kutoa rasmi matokeo, makamishna wanne wa IEBC walijitenga wakisisitiza hawatahusishwa nayo.
 
Na Jumanne, wametoa taarifa kwa vyombo vya habari wakidai hawakuhusishwa katika maamuzi ya kura za urais zilizojumlishwa.
 
Kwenye hotuba yake, Raila amehimiza wafuasi wake kudumisha amani, Azimio ikizamia njia za kisheria na Kikatiba kusaka haki.
  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Wizara ya elimu iongezee zaidi muda muhula...

BENSON MATHEKA: Viongozi wanawake waungwe mkono ili wafaulu...

T L