Habari

Raila apokea maoni kuhusu BBI huku jopokazi likienda chini ya maji

January 30th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, anaendelea kupokea maoni kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) kutoka kwa makundi kadhaa huku jopo lililotwika jukumu hilo likitoweka.

Kamati ya watu 14 inayoongozwa na Seneta wa Garissa, Yusufu Haji, imetwikwa jukumu la kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya.

Kamati hiyo ilikutana Jumatatu kwa mara ya kwanza tangu Rais Kenyatta alipochapisha rasmi majukumu yake kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

Jana, Bw Odinga alikutana na jumbe na viongozi wa maeneo tofauti kujadili BBI na jinsi wakazi wa maeneo hayo watanufaika na mpango huo.

Bw Odinga alikutana na jumbe kutoka kaunti za Narok, Kajiado na Garissa katika afisi yake ya Capital Square jijini Nairobi. Jumbe hizo zilimkabidhi orodha ya masuala ambayo yanapaswa kushirikishwa katika BBI.

“Nilipokea ujumbe wa viongozi kutoka kaunti ya Garissa kwa mazungumzo kuhusu BBI. Viongozi hao walinikabidhi masuala yanayoathiri eneo lao hasa ukosefu wa usalama ambao umeathiri elimu Kaskazini mwa Kenya,” Bw Odinga alisema kwenye taarifa.

Ni kamati inayoongozwa na Bw Haji, anayetoka kaunti hiyo ambayo inapaswa kupokea maoni yoyote ya kuimarisha ripoti iliyoandaa ambayo ilizinduliwa Novemba 27, 2019.

Gavana Joseph Ole Lenku pia alithibitisha kuwa aliongoza ujumbe wa viongozi wa kaunti za Kajiado na Narok kukutana na Bw Odinga na kumkabidhi orodha ya masuala wanayohisi yataimarisha uwiano nchini.

“Pamoja na viongozi wa kaunti ya Narok, tulikutana na Bw Odinga kushauriana kuhusu masuala yanayoathiri jamii ya Maa zikiwemo kampeni za BBI,” Bw Lenku alisema.

Mkutano wa kuvumisha BBI unatarajiwa kuandaliwa Narok Februari 17. Katika mikutano iliyotangulia Kisii, Kakamega na Mombasa, viongozi wa kisiasa walimkabidhi Bw Odinga maazimio wanayotaka yashirikishwe katika BBI, ambayo wangewasilisha kwa kamati ya Bw Haji.

Hii ilifanya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto na wale wa Bw Odinga kutofautiana kuhusu mikutano ya kuvumisha ripoti hiyo.

Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakiitaka kamati hiyo kutangaza mikutano yake ili waweze kuwasilisha maoni yao.

Jumatano, Bw Odinga alikutana na makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wakiongozwa na mwenyekiti wake Dkt Samuel Kobia kujadili BBI.