Habari MsetoSiasa

Raila apongeza kanisa la ACK kwa kukataa pesa za ufisadi

May 5th, 2019 1 min read

Na Victor Raballa

KINARA wa ODM Raila Odinga amepongeza kanisa la ACK kwa msimamo wake dhidi ya kutumiwa vibaya na viongozi wafisadi.

Bw Odinga alisisitiza kuwa kanisa halifai kutumiwa kama pahali pa kutakasa pesa za ufisadi na wanasiasa wasiotaka kufichua wanakotoa pesa za michango yao kanisani.

“Nyingi ya pesa zinazotolewa makanisani ni za ufisadi kwani zilikuwa zimepangiwa kwa ujenzi wa vifaa muhimu kama hospitali, barabara, shule na kuzalisha chakula cha kutosha kwa Wakenya,” alisema.

Kigogo huyo aliyekuwa akizungumza Siaya,lihimiza viongozi wa kidini wanaotii wito wao wasihofu kutilia shaka chimbuko la mamilioni ya pesa zinazotolewa kama michango makanisani mwao.

Bw Odinga alieleza: “Askofu Mkuu wa kanisa la Kianglikana Jackson Ole Sapit ndiye kiongozi wa kwanza wa kidini kusimama wima kuwakashifu wanasiasa wanaozunguka nchi kwa lengo la kuwahadaa Wakenya kuelekea siasa za 2022.

“Inashangaza mtu anayepokea mshahara wa Sh1 milioni kwa mwezi kutoa michango ya hadi Sh30 milioni kila mwezi.”