Habari Mseto

Raila apuuza madai kuwa amejitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais

October 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amepuuzilia habari zilizochapishwa katika gazeti moja la humu nchini Jumatatu kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mpango wa maridhiano katika ukumbi wa Bomas, Nairobi Bw Odinga hawezi kuzungumza kuhusu uchaguzi ujao wakati huu kwa sababu “kuna serikali yenye wajibu wa kuwatumikia Wakenya.”

Habari kuu katika gazeti la The Standard toleo la Jumatatu, Oktoba 26,2020 lenye kichwa “I’m in the race” (Niko kinyang’anyironi) inamnukuu Bw Odinga akisema hatastaafu na yu tayari kuwaongoza Wakenya katika kile alichokitaja kama “Ukombozi wa Tatu”.

“Wengine wanasema kuwa Baba (Raila) ni mzee, na kwamba napaswa kustaafu. Je, nistaafu au nisistaafu? Nitaendelea na juhudi za ukombozi kwa manufaa ya Wakenya; ukombozi wa tatu na wa mwisho,” Odinga akasema.

Alisema hayo Jumamosi katika kijiji cha Mabole, eneo bunge la Butere, kaunti ya Kakamega mazishi ya John Luchera, ambaye ni binamuye Gavana wa kaunti hiyo Wycliffe Ambetsa Oparanya.

Ni kauli hiyo ambayo wanahabari wa gazeti hilo walifasiri kumaanisha kuwa Bw Odinga tayari ameonyesha nia ya kuwania urais kwa mara ya tano, katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Japo Waziri Mkuu huyo wa zamani amekuwa akishikilia kuwa hanui kutumia handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta na mpango wa BBI kama ngazi ya kuwania urais 2022, bali ni kupalilia amani na utulivu nchini kuelekea uchaguzi huo.

Hata hivyo, wandani wa Naibu Rais William Ruto wamekariri kila mara kwamba handisheki na BBI ni mradi ya kumwezesha Bw Odinga kumrithi Rais Kenyatta na kuharibu mipango ya awali ya Jubilee kwamba Rais angemuunga mkono Dkt Ruto kwa kiti hicho.

Wanachama wa ODM wakiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo na kakake Odinga, Oburu Oginga, nao wametangaza bayana kuwa kinara huyo wa upinzani atania urais kwa mara nyingine 2022.