HabariSiasa

Raila arejea kwa Moi

May 6th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga na kakake Dkt Oburu Odinga Jumapili walikuwa nyumbani kwa Rais Mstaafu Daniel arap Moi, kwa ziara iliyoripotiwa kuwa ya kumpa rambirambi zao, kufuatia kifo cha mwanawe Jonathan Toroitich.

Hii ilikuwa ziara ya pili kwa Bw Odinga Kabarak, baada ya nyingine aliyofanya mwaka uliopita, wakati Mzee Moi alipokuwa ametoka kupata matibabu nchini Israel. Ziara hiyo kadhalika ilifanyika punde baada ya muafaka wa amani baina ya Bw Raila na Rais Uhuru Kenyatta.

Jan wawili hao walifika nyumbani kwa Mzee Moi, Kabarak, Kaunti ya Nakuru saa za adhuhuri ambapo walipokelewa na Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Ujumbe kutoka kwa seneta Moi ulisema kuwa viongozi hao walifika ili kumpa rais huyo mstaafu rambirambi zao za kibinafsi, baada yao kukosa kuhudhuria mazishi ya marehemu Jonathan, ambaye alizikwa nyumbani kwake Kabimoi, mnamo Aprili 27.

“Tunashukuru kama familia kwa kuwa kama watu binafsi na kama taifa mliungana nasi katika maombi wakati huo mgumu na wa kuomboleza,” ujumbe wa Bw Moi ukasema.

Ujumbe huo uliambatana na picha kadhaa ambazo viongozi hao walipiga walipofika Kabarak, wakiwa na Mzee Moi ndani ya nyumba, na nyingine wakiwa na viongozi waliokuwapo.

Wakati wa mazishi ya marehemu Jonathan, Bw Odinga alikuwa nchini China kuhudhuria kongamano kuhusu ushirikiano wa China na Afrika katika masuala ya miundomsingi.

Bw Odinga, hata hivyo, tayari alikuwa ametuma ujumbe wa pole kwa familia ya Mzee Moi wakati habari za kifo cha Jonathan zilipowekwa wazi; na pamoja na Dkt Oburu wakamtuma Seneta wa Siaya James Orengo kuwawakilisha wakati wa mazishi.

Ujumbe wa Bw Odinga baada ya ziara hiyo jana ulikuwa wa kuipa pole familia ya Mzee Moi, kisha akatuma picha sawa na alizotuma Seneta Moi katika mitandao ya kijamii.

“Tunaendelea kumtakia nguvu Rais Mstaafu na familia yake. Mungu awape amani wakati huu mgumu,” akasema Bw Odinga.

Wandani wa kisiasa wa seneta Moi Alex Tolgos (Gavana wa Elgeyo Marakwet), mbunge wa Tiaty William Kamket na Seneta Maalum Abshiro Halake, aidha, walikuwapo wakati wa ziara hiyo, kuwakaribisha viongozi hao.

Ziara za viongozi mashuhuri nchini kwa Mzee Moi Kabarak zimekuwa zikivutia hisia tofauti kisiasa, baadhi ya watu wakikataa kuzichukulia kijuujuu tu jinsi zinavyoripotiwa.

Tayari, Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga na aliyekuwa Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka wamekuwa Kabarak angalau mara mbili tangu mwaka uliopita, wakati viongozi wengine kama Naibu Rais William Ruto wakizuiwa kumwona Mzee Moi kabisa.

Juhudi za kumzuia Dkt Ruto kuonana na Rais huyo Mstaafu zilionekana kufika kilele wakati wa mazishi ya Jonathan, ambapo Mzee Moi aliepuka hafla ya mazishi iliyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kabarak- mita chache kutoka nyumbani kwake na ambapo Naibu Rais alikuwapo -lakini akahudhuria mazishi ya mwanawe eneo la Kabimoi, ambapo ni zaidi ya kilomita 50 kutoka Kabarak.