Habari

Raila arejea nchini baada ya majuma matatu akipokea matibabu Dubai

July 13th, 2020 1 min read

Na ALLAN OLINGO

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amerejea nchini baada ya majuma matatu ya kupokea matibabu Dubai; alitua Jumapili jioni.

Bw Odinga alirejea nchini kimyakimya ambapo alitumia ndege ya kifahari ya shirika la Constellation aina ya Airbus A318-112(CJ) Elite A6-CAS, MS4211.

Vyanzo kadhaa vimethibitishia Taifa Leo kwamba Odinga yuko nchini.

Mitandao inayofuatilia safari za ndege imefichua kwamba ndege hiyo ya matumizi binafsi ambayo hubeba abiria 19 ilitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumapili saa nne kasoro dakika 11 usiku.

Ndege hiyo ilikuwa imetoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum, Dubai saa kumi na moja na dakika 13

Inadaiwa ndege hiyo ilifaa kuelekea nchini Zambia hiyo Jumapili, lakini safari ikaelekezwa jijini Nairobi, kwa mujibu wa mitandao mbalimbali inayofuatilia safari za ndege.

Ilikuwa imeanza safari ya kuelekea Lusaka Jumapili asubuhi, lakini ikarudishwa Dubai wakati ikipaa katika anga ya Saudi Arabia.