Raila asaka njia mpya ya Canaan

Raila asaka njia mpya ya Canaan

WINNIE ATIENO na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, anatarajiwa kukutana na wabunge wote wa chama chake wiki hii, baada ya mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI) kugonga mwamba.

Mkutano huo pia utafanyika wakati ambapo siasa za kutafuta miungano kabla mwaka wa 2022 zimepata pigo kwa vile ilitarajiwa nafasi za uongozi katika serikali kuu zingepanuliwa kupitia kwa BBI.

Ijapokuwa ajenda ya mkutano huo haijatolewa wazi, Bw Odinga anatarajiwa kutumia mkutano huo kupanga upya mikakati kuhusu uchaguzi ujao.

“Ni wakati wa kuganga yajayo. Chama kitafanya mkutano wa wabunge wake wiki ijayo (wiki hii) ambapo tutajadiliana kuhusu hatua tutakazochukua kuendelea mbele,” Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, alithibitisha mpango wa mkutano huo akizungumza katika afisi yake Mombasa.

Bw Odinga alitoa taarifa kusema chama hicho hakitaelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, lakini alidokeza kuwa suala la kutaka marekebisho ya katiba halijafika kikomo.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, baadhi ya masuala yaliyopendekezwa katika BBI huenda yakapitishwa bungeni huku mengine yakifufuliwa baada ya 2022, hasa ikiwa waziri huyo mkuu wa zamani atafanikiwa kuunda serikali ijayo.

Alipozungumza Jumamosi akiwa katika Kaunti ya Siaya, Bw Odinga, ambaye ameashiria atawania urais katika uchaguzi ujao, alisisitiza kuwa Katiba ya sasa ambayo ilipitishwa mwaka wa 2010 ina mapengo yanayohitaji kurekebishwa.

Alitoa mfano wa pendekezo kuhusu nafasi za waziri mkuu na manaibu wao, ambazo, kulingana naye zilistahili kuwepo hata chini ya Katiba ya sasa lakini ziliondolewa wakati wadau hawakuelewana kabla refarenda ya 2010.

“Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa upishi,” akasema.

Miongoni mwa mapendekezo ya BBI ambayo huenda yakapitishwa bungeni, ni linalotaka mawaziri wawe wakichaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na vile vile, magavana waruhusiwe kuchagua mawaziri wa kaunti kutoka miongoni mwa madiwani.

Mswada kuhusu pendekezo hilo uliwasilishwa na Mbunge wa Ndaragwa, Bw Jeremiah Kioni, na bunge limekuwa likiendelea kukusanya maoni ya umma tangu Agosti 13.

Shughuli hii iliyofanywa katika maeneo tofauti ya nchi imepangiwa kukamilika leo jijini Nairobi.

Ili kupitisha masuala kama haya bungeni, wakuu wa vyama vinavyotaka marekebisho hayo watalazimika kuwaandaa wabunge ambao ni wanachama wao vilivyo.

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akishinikiza Bw Odinga aungane na vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance kuelekea kwa uchaguzi ujao.

Vinara hao ni Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula anayeongoza Ford Kenya, na Mwenyekiti wa KANU Gideon Moi aliye Seneta wa Baringo.

Hata hivyo, waliopinga mpango wa kurekebisha katiba wametaka Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta sasa wajishughulishe kuleta umoja wa wananchi.

Kulingana na Chama cha United Green Movement, mjadala mzima kuhusu marekebisho ya katiba ambao ulidumu tangu punde baada ya uchaguzi uliopita, ulisababisha mgawanyiko mkubwa wa wananchi.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bi Hamisa Zaja, alitaka changamoto sugu kama vile haki za kumiliki ardhi, ukosefu wa ajira na ugavi sawa wa rasilimali zipewe kipaumbele kabla uchaguzi ujao ufike.

“Mambo ya BBI sasa yamekwisha, tuyasahau. Wakenya bado wanakumbwa na changamoto zile zile za zamani. Inasikitisha kuwa, rasilimali zilikuwa zimeanza kusambazwa kwa kutegemea kama eneo linaunga mkono BBI au la,” akasema Bi Zaja, akiwa Mombasa.

You can share this post!

Ronaldo aachwa nje ya kikosi cha kwanza cha Juventus tetesi...

MBWEMBWE: Licha ya ukwasi wa Sh4.6b Alba aendelea kuchuma...