Habari

Raila asaliti kaunti maskini

July 28th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amewavunja moyo wafuasi wake ambao walitarajia angetetea kaunti zao kutopokonywa mabilioni ya pesa kwenye bajeti.

Akivunja kimya chake Jumatatu, Bw Odinga alienda kinyume na maseneta wa Chama cha ODM ambao walipinga mfumo mpya wa ugawaji wa pesa za kaunti utakaopelekea kaunti nyingi maskini kupokonywa pesa.

Mfumo huo ulipingwa na viongozi wa Pwani ambako ni ngome ya kisiasa ya Bw Odinga, pamoja na wale wa kaunti za kaskazini ya nchi. Walikuwa wameungwa mkono na maseneta wa kaunti nyingine kama vile Cleophas Malala wa Kakamega na Ledama ole Kina wa Narok, ambao ni wandani wa Bw Odinga.

Mfumo huo mpya uliungwa mkono pia na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, licha ya kuwa kaunti kadha za Ukambani pia zitaathirika.

Miongoni mwa kaunti zitakazopoteza pesa mfumo huo ukiidhinishwa ni kama vile Mombasa, Kilifi, Kwale, Kitui na Makueni.

Bw Odinga alieleza kuwa, Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), ndiyo imetwikwa jukumu la kuweka mfumo wa ugavi wa pesa kikatiba.

Kulingana na waziri mkuu huyo wa zamani, serikali za kaunti zimekuwa zikipoteza pesa nyingi katika ufisadi na zinafaa kukabiliana na uovu huo badala ya kutaka kutengewa pesa zaidi.

“Cha msingi katika mapendekezo hayo ni kuwa, mfumo utakaotumiwa kugawa pesa za kaunti katika miaka mitano ijayo utategemea idadi ya watu,” alisema.

Bw Odinga alisikitika kuwa maseneta wameshindwa kuelewana kuhusu mabadiliko waliyofanyia mfumo uliopendekezwa na CRA.

CRA ilipendekeza kwamba, kaunti zilizo na watu wengi zitengewe pesa nyingi. Hii itafanya kaunti 19 zilizo na idadi ndogo ya watu kupoteza Sh17 bilioni.

Mzozo ulizuka huku maseneta kutoka kaunti zitakazopoteza pesa, miongoni mwao wale wa chama cha ODM wakikataa mfumo huo huku baadhi ya wale wanaotaka kaunti zitakazofaidi wakiuunga mkono.

Kiranja wa wengi katika seneti Irungu Kang’ata alikuwa ametisha ODM kwamba upande wa serikali ukavunja handisheki iwapo hawataunga mfumo huo.

Kwa upande mwingine, viongozi wa Pwani walitishia kutounga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ikiwa mfumo huo mpya utapitishwa.

Bw Odinga alisema mzozo kuhusu mfumo huo umelemaza huduma wakati nchi inafaa kuwa imeungana kukabiliana na janga la corona linalotishia maisha na kazi za Wakenya.

Aliwaambia maseneta wakubali mapendekezo ya CRA na kuruhusu nchi kusonga mbele na maoni yanayotolewa kwa sasa yakabidhiwa tume hiyo iyazingatie itakapoandaa mfumo mwingine siku zijazo.

“Katika hali hii, itakuwa bora tukitumia mfumo ambao CRA ilipendekeza utumiwe kwa miaka mitano ijayo,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alisema mfumo wa ugawaji wa mapato unafaa kutegemea idadi ya watu kwa sababu pesa hunuiwa kuboresha maisha ya watu.

Alikubaliana na Bw Odinga kwamba, serikali za kaunti zimekolewa na ufisadi na kuwataka madiwani kuwatimua magavana ambao wanatumia vibaya pesa za umma.

Hata hivyo Naibu Rais William Ruto, alionyesha kutoridhishwa na mfumo huo akisema unaumiza baadhi ya kaunti.

“Mjadala unaondelea kuhusu mfumo wa ugawaji wa pesa za kaunti umezua mgawanyiko usiofaa. Katiba inasema wazi kuwa ugavi wa pesa zetu zote unafaa kuwa wa haki na usawa,” Dkt Ruto alisema kwenye ujumbe wa Twitter.

Alisema seneti inafaa kutafuta mfumo ambao utaridhisha kila upande bila kusababisha migawanyiko na kuumiza baadhi ya kaunti.

“Bunge ni lazima, kwa kutekeleza jukumu lake, iunde mfumo unaohakikisha usawa bila kuumiza kaunti yoyote. Inawezekana,” aliongeza Dkt Ruto.

Kwenye kikao maalumu wiki jana, maseneta walikosa kuelewana kuhusu mfumo huo na ikabidi Spika Kenn Lusaka kuahirisha kikao kikao hicho hadi leo ili pande zote zitafute suluhu.

Baadhi ya maseneta wandani wa Dkt Ruto na wale wa chama cha ODM, waliungana kukataa mfumo huo mpya.