Habari MsetoSiasa

Raila asema yeye na Uhuru hawako vyeoni kibahati

November 2nd, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amepuuzilia mbali madai kwamba yeye na Rais Kenyatta wamenawiri kisiasa kwa sababu baba zao walikuwa watawala nchini miaka ya nyuma.

Bw Odinga alisema hadhi yao imeimarika katika ulingo wa kisiasa kutoka na bidii, uvumilivu na ukakamavu wao tofauti na imani kwamba walifaidi kutokana na ushawishi wa baba zao walioshikilia nyadhifa za juu kisiasa baada ya Kenya kupata uhuru.

Rais Kenyatta na Bw Odinga ni wanawe Rais wa kwanza nchini marehemu Mzee Jomo Kenyatta na makamu wa rais wa kwanza marehemu Jaramogi Oginga Odinga mtawalia. Waliingia afisini mnamo 1963 Kenya ilipopata uhuru kutoka jwa mkoloni Mwingereza.

“Jomo Kenyatta alikuwa mtoto wa wazazi maskini. Lakini alitia bidii katika nyanja mbalimbali maishani hadi akafungwa na wakoloni kwa miaka mingi. Kwa sababu hiyo hauwezi kusema kuwa Uhuru anatawala kwa misingi kuwa babake alikuwa rais wa Kenya,” Bw Odinga akasema.

“Na Wakenya wanafahamu kuwa nimekuwa mstari wa mbele katika vita vya ukombozi wa pili wa taifa hili tangu miaka ya tisini, kilele chake ikiwa ni kupatikana kwa Katiba Mpya tunayoitumia sasa,” akaongeza.

Familia za Kenyatta na Odinga zimekuwa zikirejelewa kama za kitawala, ambazo zimewahi kushikilia nyadhifa za juu katika uongozi wa taifa hili tangu uhuru.

Bw Odinga alisema babake pia alikuwa mtoto wa maskini lakini alipanda ngazi kisiasa kutokana na bidii na uvumilivu na kujitolea kwake katika vita vya ukombozi.

“Kwa hivyo, hauwezi kusema kuwa mimi Raila ni wa familia ya kifalme. Na hakuna aliyemchagua Uhuru kwa sababu ni mwanawe Kenyatta,” akakariri.

Bw Odinga alisema hayo jana wakati wa ibada ya wafu ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake (MYWO) marehemu Jane Kiano katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Baadhi ya wakereketwa wa mabadiliko ya katiba wanapendekeza sheria ibuniwe ili kuzuia uongozi wa taifa kuzunguka kati ya familia mbili au tatu za watu mashuhuri.

Kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot mara kadhaa amekuwa akisema kuwa sheria za uchaguzi zinapasa kufanyiwa mageuzi ili kuwawezesha watu kutoka familia zisizotambulika kutwaa mamlaka.

Wakati huo huo, Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano jana ilianzisha mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya kuhusu mabadiliko ambayo wangetaka yafanyike nchini ili kukomesha ghasia za kisiasa kila baada ya uchaguzi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusufu Haji, jana ilianza kwa kupokea maoni kutoka kwa makundi mbalimbali huku ikipinga madai kuwa wajibu wake ni kubaini ikiwa Katiba inapasa kufanyiwa mabadiliko kwa kura ya maamuzi.

“Tunafahamu kuwa mjadala kuhusu kura ya maamuzi imeshika kasi. Lakini kazi yetu haina uhusiano wowote na suala hilo. Letu ni kuchukua maoni na mapendekezo ya wananchi kuhusu jinsi wanavyotaka uwiano na maridhiano yaafikiwe nchini hasa baada ya chaguzi,” Bw Haji aliwaambia wanahabari katika jumba la KICC, Nairobi