Raila ashuka bei ngomeni mwake

Raila ashuka bei ngomeni mwake

NA WANDISHI WETU

USHAWISHI wa kisiasa wa kinara wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga umedidimia kwa kiasi kikubwa katika ngome yake kuu ya Nyanza tangu kubwagwa katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.

Jumatatu, Bw Odinga alipigwa na butwaa baada ya karibu nusu ya madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kisumu kususia kikao chake jijini Kisumu.

Bw Odinga alikutana na madiwani hao kuwahimiza kuchagua Bw Elisha Oraro kuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Kisumu.

Hatua ya idadi hiyo kubwa ya madiwani kususia mkutano huo ililazimu Bw Raila kubadili kauli na kuwasihi madiwani waliohudhuria kuchagua spika waliyemtaka.

Bw Oraro aliibuka mshindi baada ya kupata kura 24 huku mpinzani wake mkuu Samuel Ong’ow akipata kura 23.

Bw Odinga alilazimika kwenda Kisumu baada ya Gavana Anyang’ Nyong’o kushindwa kushawishi madiwani kumchagua Bw Oraro ambaye alikuwa akipigiwa upatu na chama cha ODM.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa ushindi huo finyu na hatua ya baadhi ya madiwani kususia kikao cha kinara huyo wa ODM, ni ishara kwamba Bw Odinga ameanza kupoteza ushawishi wa kisiasa katika eneo la Luo Nyanza.

Huku Bw Odinga akiendelea kupoteza umaarufu katika ngome yake, wanasiasa waliomuasi na kuunga mkono Rais William Ruto wamegeuka kivutio cha wengi.

Wandani wa Rais Ruto ambao umaarufu wao umeongezeka katika eneo la Nyanza ni aliyekuwa gavana wa Migori, Okoth Obado, mwanauchumi Eliud Owalo, kiongozi wa chama cha MDG, David Ochieng na mbunge wa zamani wa Rarieda, Nicholas Gumbo.

Bw Gumbo alitia saini mkataba wa kuungana na chama cha UDA, kinachoongozwa na Rais Ruto mara baada ya kubwagwa katika ugavana Kaunti ya Siaya.

Siku chache baadaye, mbunge wa Ugenya Bw Ochieng, aliyekuwa Seneta wa Kisumu Fred Outa, gavana wa zamani wa Kisumu Jack Ranguma na aliyekuwa mbunge wa Kisumu Magharibi, Olago Aluoch pia walitangaza kuunga mkono Rais Ruto.

Wandani hao wa Rais walisema Jumatano kuwa wamekuwa wakihangaishwa kwa simu na wafanyabiashara na wanasiasa kutoka Nyanza wanaosaka kazi katika serikali ya Dkt Ruto.

Mabw Obado, Owalo, Ranguma na Aluoch wana matarajio ya kutunukiwa nyadhifa na Rais Ruto atakapotangaza baraza lake la mawaziri wiki ijayo.

“Mimi sikuunga mkono Dkt Ruto ili kupata wadhifa. Lengo langu kuu ni kuleta maendeleo katika eneo la Nyanza,” Bw Obado aliambia Taifa Leo.

Rais Ruto anatarajiwa kupokea wanasiasa zaidi kutoka Luo Nyanza atakapozuru jiji la Kisumu wikendi hii kushuhudia hitimisho la makala ya 94 ya tamasha ya muziki ya shule za msingi na sekondari.

Wanasiasa katika eneo la Nyanza wameanza juhudi za kutaka kumrithi Bw Odinga anayetarajiwa kustaafu siasa.

Gavana wa zamani wa Nairobi, Dkt Evans Kidero tayari amezindua chama chake cha Democratic Congress Party kujiandaa kuchukua nafasi ya ODM.

Mbali na kupoteza umaarufu katika eneo la Nyanza, Bw Odinga pia anakabiliwa na kibarua kigumu cha kudhibiti na kuunganisha chama cha ODM.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi amekuwa akilalamikia Bw Odinga kwa ‘kumsaliti’ baada ya kukosa kumpa wadhifa wa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

Kulingana na Bw Mbadi, wadhifa huo aliopewa mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi ulifaa kuwa wake kwani alijitoa mhanga kwa kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay baada ya Bw Odinga kumtaka kumwachia Gavana Gladys Wanga. Hata hivyo yafaa kueleweka mrengo unaounda serikali – wa Kenya Kwanza – nao unadai kuwa ndio unaofaa kutwaa nafasi hiyo ukiwa tayari umempendekeza mbunge wa Kikuyu Bw Kimani Ichung’wa.

Wabunge wa ODM waliohojiwa na Taifa Leo pia wameelezea kulegeza msimamo wao Bungeni licha ya Bw Odinga kuwataka kukosoa na kukaa ngumu dhidi ya serikali ya Rais Ruto.

“Hakuna haja ya sisi upinzani kukalia ngumu serikali ya Ruto. Acha serikali ifanye inavyotaka ndipo Wakenya wajue uchungu wa kumchagua,” akasema Bw Mbadi.

Wabunge wa ODM pia wamekuwa wakipinga chini kwa chini pendekezo la Bw Odinga kutaka kuandaa maandamano kushinikiza mageuzi ndani ya Idara ya Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Odinga wiki iliyopita alitishia kufanya maandamano dhidi ya asasi hizo mbili lakini pendekezo hilo limepingwa vikali na viongozi wa vyama tanzu vya Azimio kama vile Wiper na Jubilee.

Ripoti za Rushdie Oudia, Victor Rabala na Leonard Onyango

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: MCAs wafanye hima kuwapa Wapwani matunda...

Mradi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakwama Mukuru

T L