Maoni

Raila asiende AU, Gen Z watampa Urais vizuri 2027

Na CECIL ODONGO July 8th, 2024 2 min read

KINARA wa Azimio Raila Odinga anastahili kughairi nia yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na kuendea Urais mnamo 2027.

Makabiliano kati ya vijana barobaro maarufu kama Gen Z na serikali yanayoendelea nchini ni nafuu kisiasa kwa kiongozi huyo wa upinzani.

Raila amekuwa katika siasa za upinzani kwa kipindi kirefu akipambana kukomboa nchi hii lakini mara nyingi ameshindwa katika njia tatanishi na kupigwa vita vya kikabila.

Katika uchaguzi mkuu wa 2007, kiongozi huyo wa upinzani nusura aingie Ikulu na kutekeleza mabadiliko ya uongozi aliyoyataka. Hata hivyo, mizozo ya kisiasa iliyoishia ghasia ilichangia kuundwa kwa serikali ya muungano kati yake na Mwai Kibaki.

Kwa mujibu wa Bw Odinga, alipokonywa ushindi katika chaguzi za Urais 2013, 2017 na 2022. Wengi wa wafuasi wa Raila wamekuwa wakiamini kuwa ndiye mwanasiasa pekee ambaye anaweza kuleta mabadiliko nchini kutokana na dhuluma ambazo amepitia akipigania ukombozi.

Miezi mitatu iliyopita, Waziri Mkuu huyo wa zamani alitangaza kuwa analenga kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa AUC ambao kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki.

Hata hivyo, kwa utathmini wangu, matukio ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa nchini yanaonyesha kuwa Raila sasa anasakwa na urais wala si yeye anautafuta kama zamani.

Mwanzo, Ma Gen Z wameonekana kutambua juhudi za ukombozi za Bw Odinga ambazo zilianza hata kabla ya baadhi yao kuzaliwa ndiposa walimwambia akae kando na awaachie wayachukue majukumu ya kulaninisha mambo.

Vijana hao wamefanikiwa pakubwa kwa sababu hawana miegemeo ya kikabila.

Hapo awali, wakati Raila alipokuwa akiongoza maandamano ya kukomboa raia, alirejelewa kama kiongozi mkabila ambaye alikuwa akipigania jamii yake tu.

Hata hivyo, vijana baada ya kusukumwa sana pembeni na sera hasi za kiuchumi ambazo zimesababisha maisha yawe magumu, sasa wanaona kuwa kile Raila alikuwa akipigania kilikuwa na mashiko.

Iwapo vijana wanambua juhudi za Raila, basi ni dhahiri akiwaomba wamuunge mkono na ukabila usiwe, basi ‘Baba’ atakuwa pazuri kuingia Ikulu mnamo 2027.

Pili, hawa vijana wa Gen Z wameapa kuwa watajisajili kama wapigakura na kufanya maamuzi makubwa katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Wamekerwa na utendakazi wa Rais William Ruto kiasi kuwa wengi wanasema hawawezi kumrejesha uongozini mnamo 2027.

Kama vijana tayari wameamua kumpa kisogo Rais Ruto, kiongozi gani ana tajriba ambaye anaweza kuchukua uongozi wa nchi kuliko Bw Odinga?

Iwapo Gen Z watachukua kura kwa wingi na wampigie ‘Baba’ basi itakuwa vigumu kwake kushindwa na Rais Ruto hata kwa kura chache jinsi ilivyokuwa 2022.

Mjadala kuwa Gen Z wanaweza kutumia idadi yao kumchagua mwenzao bado haionekani itawafaa pengine tu wamchague atakayekuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga.

Mgombeaji mwenza huyo anaweza kujifunza masuala ya uendeshaji wa nchi na kuhakikisha matakwa ya vijana yanatimizwa, kabla ya kuchukua usukani mnamo 2032.

Hoja hizo zote zinaonyesha Raila atakuwa chaguo la wengi mnamo 2027 na atakuwa akipoteza nafasi tukizi akiamua kuendea uenyekiti wa AUC ambao hauwezi kulinganishwa na Urais.