Raila asihi wafuasi wake wajitokeze kwa wingi wamuingize Ikulu

Raila asihi wafuasi wake wajitokeze kwa wingi wamuingize Ikulu

NA SAMMY WAWERU

ZIMESALIA siku mbili pekee taifa lishiriki uchaguzi mkuu, utakaofanyika Jumanne, Agosti 9.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imehakikishia Wakenya kwamba imejiandaa kuendesha uchaguzi kwa njia iliyo huru, ya haki na yenye uwazi.

Ikiwa leo Jumamosi, Agosti, 6 ndiyo siku ya mwisho kwa viongozi wanaomezea viti vya kisiasa, kinara wa Azimio One Kenya Alliance, Raila Odinga amefanya mkutano wa mwisho katika Uwanja wa Kimataifa wa Safaricom Kasarani, jijini Nairobi.

Mkutano huo wa maombi, umehudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa kiongozi huyo wa ODM aliyeandamana na mgombea mwenza, Bi Martha Karua (Narc Kenya).

Katika hotuba yake iliyosheheni sera na ahadi chungu nzima kukomboa uchumi wa Kenya endapo atambwaga mpinzani wake, Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza, Bw Odinga amewataka wanaomuunga mkono kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.

“Siku ya siku, tupulize vipenga viwili; Moja ni ya kuwatimua mafisadi na adui wa nchi, na nyingine kuamsha watu waende katika vituo vya kura kunichagua,” akasema Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Odinga anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta, wawili hao wakiridhia uhusiano wao wa karibu baada ya kutangaza kuzika tofauti zao kisiasa Machi 2018, kupitia salamu za maridhiano almaarufu Handisheki.

“Mimi na Rais Mstaafu Daniel Arap Moi akielekea kuondoka mamlakani, na 2008 na Rais Mwai Kibaki ambaye pia ni Mstaafu (wawili hao wakiwa marehemu kwa sasa), nilifanya salamu za maridhiano na viongozi hao. Machi 2018, niliridhiana na ndugu yangu, Rais Uhuru Kenyatta.

“Vitendo hivyo vinaashiria mapenzi niliyo nayo ya nchi hii, na ndio maana ninawaomba mnichague kama Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya,” Bw Odinga akaelezea.

Mbali na Odinga na Dkt Ruto, wengine watakaokuwa debeni kuwania urais ni Bw David Mwaure (Agano Party) na Prof George Wajackoyah wa Roots Party.

  • Tags

You can share this post!

Soko China: Kilimo cha avokado kunoga nchini Kenya

Arsenal wakomoa Crystal Palace katika mechi ya kwanza ya...

T L