Raila asuka njama ya kumzima Ruto Pwani

Raila asuka njama ya kumzima Ruto Pwani

Na MAUREEN ONGALA, WINNIE ATIENO na WACHIRA MWANGI

CHAMA cha ODM kimeandaa mikakati maalumu ambayo viongozi wake wanaamini itasaidia kuepusha umaarufu wake kufifia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Huku uchaguzi ujao unapokaribia, chama hicho kimekumbwa na changamoto mbalimbali katika ukanda wa Pwani.Chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, kinakumbwa na ushindani kutoka kwa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kando na baadhi ya vyama ambavyo vina mizizi ukanda wa Pwani.

Baadhi ya wafuasi wa ODM walihamia UDA huku wengine wakiashiria kuhamia chama kipya cha Pamoja African Alliance (PAA) ambacho kinaongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi.Maafisa wa ODM katika kaunti za Pwani, wamesisitiza matukio hayo hayawababaishi kwani kuna mipango ya kuziba nyufa kabla uchaguzi ujao ufike.

Imebainika kuwa, miongoni mwa mipango ambayo ODM inataka kutumia kuelekea 2022 ni kuhakikisha wagombeaji viti watakaoteuliwa ni watu wanaoweza kushinda uchaguzini, kuvutia vyama vidogo vya Pwani upande wake, na kuondoa watu wasio waaminifu chamani.

Kando na hayo, chama hicho pia kinafanya kila juhudi kuepusha migawanyiko ambayo kwa kawaida hutokea baada ya kura za mchujo, na kuangazia changamoto mpya zinazokumba Wapwani kando na nyingine ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi.

Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, alifichua wikendi kwamba tayari kuna mashauriano kumshawishi Bw Odinga aangazie changamoto ambazo ziliibuka miaka ya hivi majuzi ikaathiri uchumi wa Pwani.Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa tatanishi baina ya serikali ya kitaifa na kaunti za Pwani tangu ugatuzi ulipoanzishwa 2013, ni kama vile ugavi wa mapato ya bandari ya Mombasa, usimamizi wake, na agizo kuwa mizigo yote inayoelekea Nairobi isafirishwe kwa reli ya SGR.

Hii ni kando na changamoto ambazo zimekuwepo tangu jadi, kama vile tatizo la umiliki wa ardhi ambalo hutumiwa katika kampeni kila mara bila suluhisho kupatikana.“Ni lazima Mombasa ihesabiwe kama eneo huru kiuchumi. Lazima tuwe na makubaliano mapya,” akasema gavana huyo aliye pia Naibu Kiongozi wa ODM kitaifa.

Tangu baada ya uchaguzi wa 2017, ODM iliwaadhibu wanasiasa wengi Pwani walioamua kuchukua mwelekeo tofauti na ule wa chama.Miongoni mwao ni Bw Kingi aliyepokonywa wadhifa wa Mwenyekiti wa chama Kilifi, na wabunge kama vile Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambao chama kilitaka kuwaondoa kwenye sajili yake na kuwapokonya nyadhifa katika kamati za bungeni.

Mwenyekiti wa ODM, tawi la Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alisema chama hicho sasa kiko makini kuhusu wanachama watakaodhaminiwa kuelekea 2022. Ili kujisuka kama chama kinachojali maslahi ya Wapwani kuliko vingine, ODM pia inaendeleza mashauriano na vyama vya Pwani ili kuunda muungano pamoja.

“Vyama kadhaa vya Pwani vimeonyesha nia ya kutaka kushauriana na ODM. Bado tunaendeleza mipango hiyo kimyakimya,” akasema Bw Mwambire.Wakati wa ziara yake Pwani hivi majuzi, Bw Odinga alifanya mikutano na wanasiasa wanaotaka tikiti ya ODM kuwania viti mwaka ujao akasisitizia kuhusu hitaji lao kubaki ndani ya chama hata kama hawatafanikiwa kupata tikiti.

Chama hicho kinalenga kutilia maanani zaidi wagombeaji ambao wana umaarufu na uaminifu kwa chama, na huenda kisitumie kura ya mchujo kuamua wagombeaji katika baadhi ya maeneo.Hata hivyo, inatarajiwa kuwa watakaoshawishiwa kuachia wenzao nafasi wataahidiwa nafasi nyinginezo endapo ODM itafanikiwa kuunda serikali ijayo.

“Kama tuna umoja, hakuna jambo litakalotushinda. Tunachofaa kufanya ni kuhakikisha tunatetea chama chetu,” Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Khamis, alisema wikendi.ODM imeonekana kulenga kuwavutia wanasiasa wote wanaoaminika kuwa na ushawishi wa kisiasa upande wake, kama mbinu ya kuvuruga maazimio ya wapinzani wa Bw Odinga.

Baadhi yao ni mfanyabiashara Suleiman Shahbal na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi Gideon Mung’aro ambao waliibuka wa pili kwa kinyang’anyiro cha ugavana 2017, Kaunti za Mombasa na Kilifi mtawalia

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Jamii zirejelee misingi ya malezi bora...

Msifute watu sababu teknolojia, Chelugui asihi

T L