Raila ataka kesi za kupinga BBI zitupiliwe mbali

Raila ataka kesi za kupinga BBI zitupiliwe mbali

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, ameiambia mahakama kwamba kesi zilizowasilishwa dhidi ya Mpango wa Maridhiano (BBI) zina nia mbaya na zimewasilishwa kimakusudi ili kusambaratisha mchakato huo.

Hayo yamejiri huku mabunge ya kaunti yaliyopitisha mswada wa marekebisho ya katiba yakifika kumi.Jana, kaunti za Nairobi, Kisii, Laikipia na Vihiga zilijiunga na Siaya, Kisumu, Kajiado, West Pokot, Busia, Trans Nzoia na Homa Bay zilizotangulia.

Akiwa pamoja na Kamati ya Kitaifa Shirikishi kuhusu mchakato huo, Bw Odinga alisema kesi saba ambazo zimewasilishwa dhidi ya mpango huo hazilengi kutafuta haki, bali lengo lake kuu ni kutimiza malengo ya kisiasa ya watu fulani.Hivyo, aliliomba jopo la majaji watano wanaosikiliza kesi hizo kuzifutilia mbali, akizitaja kuwa ni za kuipotezea muda mahakama.

Zaidi ya hayo, alisema zinaingilia uhuru wa Bunge la Kitaifa, mabunge ya kaunti na Seneti.Kupitia wakili Paul Mwangi, Bw Odinga anasema kesi hizo pia zinavuruga utaratibu ufaao wa kisiasa, kwani walioziwasilisha wanaitaka mahakama “kuingilia kati na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa na Bunge, Afisi ya Rais na wananchi kwa jumla.”

“Hakuna ushahidi wenye uzito uliowasilishwa kuonyesha mchakato wa BBI unapaswa kusitishwa kwa msingi wa kutozingatia sheria ama kukiuka utaratibu wa kuibadilisha Katiba,” akasema Odinga.

Kiongozi huyo pia alishangaa kwa nini walalamishi walikosa kuwasilisha kesi kupinga mipango ya awali ya mageuzi ya katiba kama Punguza Mzigo mnamo 2017 na Okoa Kenya, ulioendeshwa na muungano wa Cord.

“Kesi hizi hazina msingi wowote kwani walalamishi wanaendeleza mashtaka yao kiubaguzi ili kuhakikisha mchakato huu hautafaulu. Sababu kuu ni kwamba hakuna yeyote kati yao aliyewasilisha kesi kupinga harakati za awali za kubadili Katiba,” akasema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dennis Waweru, alikosoa kauli ambazo zimewasilishwa na mwanauchumi David Ndii na wanaharakati wengine wanne kuwa sehemu nne za Katiba ya sasa haziwezi kufanyiwa mageuzi yoyote—kupitia Bunge la Kitaifa ama kura ya maamuzi.

Wanaharakati hao wanasema Sehemu ya Kwanza, Pili, Nne, Tisa na Kumi za Katiba haziwezi kufanyiwa mabadiliko yoyote.Hata hivyo, Bw Waweru alisema kuwa Katiba ni nakala ambayo inaweza kufanyiwa mageuzi wakati wowote, kwa msingi wa vipengele 255, 256 na 257 mtawalia.

“Ikiwa wale walioitengeneza Katiba hawakutaka lolote kubadilishwa, basi wasingeweka sehemu zinazoeleza taratibu zinazofaa kufuatwa katika kuibadilisha,” akasema Bw Waweru, huku akirejelea Sehemu 16 ya Katiba, yenye anwani ‘Taratibu za kuifanyia mabadiliko katiba hii.’

Kwenye kesi hiyo, Dkt Ndii na wanaharakati Jerotich Seii, James Ngondi, Wanjiku Gikonyo na Ikal Angelei wanasema sehemu hizo ndizo msingi mkuu wa Katiba, na haziwezi kufanyiwa mabadiliko kupitia Bunge au kura ya maamuzi.

Hata hivyo, Waweru alisema wanaharakati hao wanakita kauli zao kwenye miundo ya katiba za kigeni, hali ambayo ni tofauti sana na Katiba ya Kenya.Ripoti za Joseph Wangui, Derick Luvega, Collins Omulo na Wycliffe Nyaberi

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: DCI ijitahidi kung’amua mbinu za wizi...

Serikali yaonya mvua yaja mwezi ujao kwa kishindo kikuu