Raila atakiwa aandamane na Uhuru ziara ya Mlima Kenya

Raila atakiwa aandamane na Uhuru ziara ya Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI

WAFUASI wa vuguvugu la Azimio la Umoja wamemtaka kinara wa ODM Raila Odinga kuandamana na Rais Uhuru Kenyatta atakapozuru eneo la Mlima Kenya wiki ijayo.

Mwenyekiti wa madiwani wa kaunti za Mlima Kenya Bw Charles Mwangi jana alisema kuwa Bw Odinga atajipatia ufuasi mkubwa katika eneo hilo endapo ataandamana na Rais Kenyatta.

Bw Odinga anatarajiwa kukita kambi katika eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a Januari 29.

“Bw Odinga akiandamana na Rais ataonekana akiwa na nguvu za ziada. Sisi tumemkubali azuru Mlima Kenya na mimi binafsi nitahudhuria mikutano yake yote,” Bw Mwangi aliambia Taifa Leo.

Licha ya kuashiria kuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake atakapostaafu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Rais Kenyatta hajawahi kuandamana na kiongozi wa ODM katika eneo la Mlima Kenya ambayo ni ngome yake ya kisiasa.

Ziara hiyo ya Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya inalenga kupunguza umaarufu wa Naibu wa Rais William Ruto.

Dkt Ruto baada ya kujipigia debe Mlima Kenya kwa zaidi ya miaka minane wakati wa serikali ya Jubilee, anaonekana akiwa na guu mbele eneo hilo.

Mkutano huo wa Kiharu unatarajiwa kuwasha joto la kisiasa haswa ikizingatiwa kuwa mbunge wa eneo hilo Bw Ndindi Nyoro ni mfuasi sugu wa Dkt Ruto.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth, anasema kuwa mkutano huo wa Murang’a utakuwa mwanzo wa kampeni kali ya kumaliza ushawishi wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

“Ili kuanza kubadili dhana kwamba Mlima Kenya ni ngome ya Dkt Ruto, tumelenga kuandaa mikutano mikubwa ya kisiasa vijijini ambapo tutaonyesha dunia nzima kwamba Bw Odinga ndiye atamrithi Rais Kenyatta,” akasema Bw Kenneth.

Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata, hata hivyo, anasema kuwa Bw Odinga ako na kibarua kigumu katika safari yake ya kusaka umaarufu Mlima Kenya ikizingatiwa kwamba ametiwa uvundo mkuu eneo hilo na ambao atahitaji ‘muujiza’ kujiosha.

“Zile shaka kuhusu Bw Odinga na wafuasi wake ambazo zimepandwa katika fikira za wenyeji kwa miongo minne sasa sio suala la kurekebishwa na mikutano ya miezi saba…Lakini anakaribishwa Mlima Kenya, atatunzwa na atasikizwa lakini ajue anapoteza wakati wake,” akasema Bw Kang’ata.

Bw Nyoro alisema kuwa ana fununu kwamba Bw Odinga ataandaa mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Ihura na pia ahutubie umma katika mikutano kadhaa akiingia na akitoka katika eneo hilo. Aliongeza kuwa Bw Odinga yuko huru “kuja Murang’a na Mlima Kenya kupoteza wakati wake wa kisiasa kwa kuwa hawezi kujinusuru kutoka kwa hasira ya wapiga kura wa Mlimani kufuatia siasa zake za ghasia.”

Bw Stanley Karuri ambaye anawania Useneta wa Murang’a kwa chama cha ODM aliwataka wawaniaji wengine wakome uoga wa kujihusisha na chama hicho.

“Nawaomba wote ambao tuko katika ufuasi kwa Bw Odinga tuingie katika chama cha ODM badala ya kujificha katika vyama mbadala kama fuko,” akasema.

Katibu Mkuu wa chama cha Dkt Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) Bi Veronica Maina aliambia Taifa Leo kwamba “kunao wanaojifanya kuwa wanatuunga mkono lakini hawaingii chama chetu.”

Alisema kuwa wengi wa wafuasi wa Bw Odinga wanajipenyeza katika vyama vya Mlima Kenya na kuhadaa wenyeji kuwa wanamuunga mkono Dkt Ruto ilihali wao ni maajenti wa Azimio la Umoja.

Bi Maina aliwatahadharisha wenyeji wa Mlima Kenya wawe makini sana wanapojihusisha na baadhi ya wanasiasa ambao wanajipigia debe nje ya chama cha UDA.

Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi aliambia Taifa Leo kwamba Bw Odinga anapenyezwa Mlima Kenya na Rais Kenyatta na pia mabwanyenye na wanasiasa walio na tajiriba ya siasa za eneo hilo.

“Katika siku zijazo, utaona Bw Odinga akikubalika kwa kasi eneo hili na kilele cha siasa zake akishirikiana na Rais ni pale mmoja wetu atatawazwa kuwa mgombezi mwenza ili atuwakilishe katika serikali ijayo akiwa Naibu wa Rais,” akasema.

Bw Kang’ata alisema kuwa Bw Odinga anatumiwa tu na madalali wa kisiasa ambao nia yao kuu ni kuunda pesa kutokana na hifadhi ya kampeni zake ambayo inaandaliwa na Rais na Serikali yake, mabwanyenye wa Mlimani pamoja na ngome zake za jadi nje ya Mlima, Mataifa ya kigeni pamoja na ukwasi wake binafsi.

“Hawamwambii kwamba akikosa kuteua mgombezi mwenza wake kutoka Mlima Kenya basi hataungwa mkono na wapiga kura wa eneo hili. Na pia, akiteua mmoja wetu kuwa mgombezi mwenza, atapoteza kura nyingi ambazo zimekuwa zikimwendea kutoka eneo la Ukambani ambako amekuwa akiteua Bw Kalonzo Musyoka kama msaidizi wake wa kusaka kura,” akasema.

Kamishna wa eneo la kati anayeondoka Bw Wilfred Nyagwanga alisema kuwa usalama umeimarishwa katika safu ya kisiasa ili kuzima hali za ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa wakati wafuasi wa mirengo ya Dkt Ruto, Rais Kenyatta na Bw Odinga imegongana katika mikutano ya hadhara, kwingine ikizua maafa.

“Ziara za Bw Odinga eneo la Kati ni halali na pia zile za wawaniaji wengine wote. Kauli yetu kama maafisa wa kiusalama ni demokrasia ipewe nafasi ya kutanda na wapiga kura wajiamulie kwa hiari yao bila ya kuwekwa katika makundi ya makabiliano,” akasema.

Mwenyekiti wa bodi ya Kampeni za Bw Odinga aliye pia gavana wa Laikipia Bw Ndiritu Miriithi alisema kwamba “meli ya Azimio imeng’oa nanga katika eneo la Mlima Kenya na itazua mawimbi ya msisimko katika kila pembe na bila shaka ile asilimia tatu ambayo humwendea Bw Odinga katika chaguzi tangulizi itapanda hadi 50.”

Alisema Rais Kenyatta atatumia ushawishi wake kuhakikisha urithi wake Mlimani umemwendea aliyemtii akiwa ni aidha Bw Kenneth, Waziri wa Kilimo Bw Peter Munya au mwingine yeyote ambaye ako na maono pana ya umoja na ustawi wa kitaifa.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau ambaye ni mfuasi sugu wa Bw Kenneth alisema kuwa “rais ametuhakikishia kwamba Bw Odinga ndiye pendekezo lake na kile tunafaa kufanya ni kuunda kambi yetu ya wafuasi na tuingie mashinani kuunga mkono Azimio.”

  • Tags

You can share this post!

Shule zakandamiza wazazi kwa kuwatoza ada za ziada zisizofaa

Viwanda vyafungwa mahindi yakikosekana

T L