Makala

Raila atangaza kuondokea siasa za Kenya, akimezea mate wadhifa wa Afrika  


ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Bw Raila Odinga, Jumatano, Agosti 21, 2024 alitangaza kwamba amejiondoa kutoka siasa za Kenya na kuingia katika siasa za Bara la Afrika katika juhudi zake za kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Bw Odinga alisemna kuwa hatajishughulisha sana na siasa za Kenya kuanzia sasa ili kuangazia kampeni zake za wadhifa wa Bara.

Akizungumza wakati wa kikao cha pili na wanahabari pamoja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi jijini Nairobi, Bw Odinga alisema atawekeza juhudi zote katika kampeni zake baada ya kuwasilisha rasmi ombi la kuwania uenyekiti wa AUC.

“Nitaanza kufanya kazi barani mara tu nitakapochaguliwa na hiyo itakuwa Februari mwaka ujao, 2025.

“Kwa sasa ninahusika katika kampeni lakini hiyo haimaanishi kuwa Kenya itakoma kuwepo,” Bw Odinga alisema.

Aliendelea: “Sitashiriki sana katika siasa za Kenya kuanzia  sasa ninapoendelea kuelekeza mawazo yangu katika kampeni ya bara. Lakini ni kipindi cha mpito kutoka kushiriki kikamilifu siasa za Kenya hadi siasa za bara la Afrika,” alisema.

Jumanne, Agosti 27, 2024 Rais William Ruto atamtambulisha rasmi waziri mkuu huyo wa zamani kama mgombeaji wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano  wa Afrika (AUC) na kuzindua rasmi  kampeni zake kote barani.

Bw Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Wakenya walio ng’ambo mnamo Jumatano Agosti 21, 2024 alitangaza kwamba Dkt Ruto atatoa ratiba rasmi ya kampeni ya Raila.

Bw Mudavadi alisema azma ya Bw Odinga kuwania wadhifa wa juu wa bara ni “shughuli ya kitaifa.”

“Hii ni zaidi ya ugombeaji tu; ni shughuli ya kitaifa. Mheshimiwa Raila Odinga anawakilisha sauti, maadili na matarajio ya Kenya katika bara hili. Anaposonga mbele, tusimame naye, si tu kama serikali bali kama watu walioungana,” Bw Mudavadi alisema.

Aliwataka Wakenya kumuunga mkono kiongozi huyo wa ODM.

“Kwa Wakenya wenzangu, kama taifa, kila mara tunaungana ili kusimama nyuma ya mmoja wetu, iwe kwenye nyimbo, uwanjani, au kwenye jukwaa la kimataifa. Kama tulivyoshangilia wanamichezo wetu katika michezo ya Olimpiki ya hivi karibuni, tumuunge mkono kikamilifu Mheshimiwa Raila akibeba bendera ya Kenya juu katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.”

Bw Mudavadi alisema kuwa Rais Ruto atazindua rasmi timu ya kampeni ya Bw Odinga, na kuongeza kuwa sekretarieti hiyo itatayarisha kampeni kali kote barani.

Baadhi ya wapanga mikakati wa Bw Odinga ni pamoja na; aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika Elkanah Odembo, aliyekuwa katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) Mahboub Maalim, Balozi Anthony Okara, Prof Makau Mutua na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nyeri Dkt Caroline Karugu.

Bw Mudavadi alisema kuwa katika ombi lake la kutaka kuwa mwenyekiti wa AUC, Bw Odinga alieleza maono yake kwa muungano huo wa kanda ambayo alibainisha kuwa yanaegemea nyanja mbalimbali zikiwemo ushirikiano wa Afrika na maendeleo ya miundombinu, mabadiliko ya kiuchumi Barani Afrika, kuimarisha biashara Afrika, uhuru wa kifedha, mabadiliko ya kilimo, hatua za hali ya hewa, amani na usalama, uwezeshaji wa vijana, na usawa wa kijinsia.

Bw Odinga alisema anafurahi kwamba serikali ya Kenya imemfanya kuwa mgombea wake rasmi.