Raila atangaza Machi 20 kuwa siku ya mapumziko

Raila atangaza Machi 20 kuwa siku ya mapumziko

NA WINNIE ONYANDO

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, ametangaza Jumatatu, Machi 20 kuwa siku ya mapumziko ili kuwapa wafuasi wake muda wa kujumuika na kuandamana pamoja jijini Nairobi.

Akizungumza Jumanne katika mkutano wa kisiasa Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema siku hiyo itakuwa ya kipekee wafuasi wake wakiandamana Nairobi kupinga serikali ya Rais William Ruto.

“Tunatangaza kwamba Jumatatu, Machi 20 itakuwa siku ya mapumziko,” akasema Bw Odinga.

Haya yanafuata wito wa Kiongozi wa NARC Kenya, Martha Karua, aliyemtaka Bw Odinga kutangaza siku hiyo kuwa ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa Wakenya kuhudhuria maandamano hayo makubwa.

“Tunakuomba kwa unyenyekevu uifanye siku hiyo kuwa ya mapumziko. Hatuwezi kuendelea kukumbatia masuala ya uwizi wa kura kila mwaka. Tunataka ukweli ujulikane,” alisema Bi Karua.

Kiongozi wa Upinzani hana mamlaka ya kutangaza siku ya kitaifa ya mapumziko. Kikatiba, jukumu hilo limetwikwa Waziri wa Usalama wa Ndani ambaye pia anahitajika kutangaza hayo kupitia chapisho kwenye gazeti la serikali, Kenya Gazette.

Na Jumanne, Bi Karua alisisitiza kuwa Azimio ilishinda kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Bi Karua alisema wito huo unanuia kuwanufaisha wapiga kura ambao alisema wanafaa kujua ukweli.

Kwa upande wake, Bw Odinga alisema siku hiyo Wakenya watajumuika jijini Nairobi kuandamana barabarani kupinga serikali ya Rais Ruto.

“Kumbuka Machi 20, 2023, tutakutana jijini Nairobi. Siku hiyo, wafuasi wetu kote nchini watafanya maandamano makubwa Nairobi,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga amekuwa na misururu ya mikutano ya kisiasa katika kaunti mbalimbali akiwashinikiza wafuasi wake kupinga serikali ya Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa tosti ya viazi vitamu na...

Jicho Pevu aponea shambulio la risasi

T L