Raila atarajiwa Githurai kupigia debe BBI

Raila atarajiwa Githurai kupigia debe BBI

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga anatarajiwa kuingia Githurai wakati wowote kuanzia sasa leo Jumatano kupigia debe Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Baadhi ya wafanyabiashara wameogopa kufungua maduka na vibanda vyao, wakihofia mali yao kuporwa na kuharibiwa.

“Tuliarifiwa Baba anakuja Githurai leo na joto limepanda ikisemekana kando na BBI atazungumzia soko jipya linaloendelea kutengenezwa, na ambalo lina malumbano,” Samson Gitau ambaye ni mmiliki wa duka la M-Pesa ameambia Taifa Leo.

Kulingana na mfanyabiashara huyo na ambaye amefungua duka lake ingawa kwa wasiwasi, hoja kuu si ziara ya Bw Raila kupigia upatu BBI, ila ni suala tata la soko.

Inasemekana kuna baadhi ya wahuni wanaotaka kulinyakua litakapozinduliwa, ilhali linajengwa kwa minajili ya wafanyabiashara wa soko la Jubilee ambao huendeleza biashara zao katika ardhi ya Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini (KenHA) na itakayoundwa egesho la magari.

“Tumegundua kuna matapeli kutoka soko la Migingo, lililoko Githurai karibu na reli, wanaotaka kujinyakulia soko tuliloahidiwa kama Wanajubilee, hatutakubali hadaa za aina hiyo. Tumeambiwa wao ndio wamealika Raila Odinga,” akadai mfanyabiashara mwingine.

Vibanda na maduka mengi ya Soko la Jubilee vimesalia mahame.

Maafisa wa polisi waliojihami kwa gesi ya vitoa machozi wanaendelea kupiga doria Githurai na viunga vyake.

Bw Raila amekuwa akizuru maeneo mbalimbali nchini kufanyia kampeni BBI, na ambayo inapendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho.

 

You can share this post!

Maafisa wa DCI wamkamata mwanamume anayeshukiwa kumuua...

Arsenal wapepeta Southampton na kutinga ndani ya orodha ya...