Habari MsetoSiasa

Raila atasalia kwa siasa licha ya kuteuliwa AU – Wachanganuzi

October 22nd, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga hataacha kufanya siasa nchini licha ya kuteuliwa Mjumbe wa Muungano wa Afrika (AU), wachanganuzi wa siasa wanasema.

Bw Odinga aliteuliwa Mjumbe wa AU kuhusu Miundomsingo na Mwenyekiti wa AU Moussa Mahamat, ambaye walikutana jijini Addis Ababa, Ethiopia kabla ya tangazo hilo.

Wanaoteuliwa katika cheo cha ngazi hiyo ya juu katika AU huwa ni viongozi mashuhuri waliostaafu kama vile marais, mawaziri wakuu na wakuu wa majeshi, na uteuzi wa Bw Odinga ulionekana na baadhi ya watu kama ishara yake kuacha siasa.

Kiongozi huyo wa upinzani sasa atakuwa na ofisi mjini Addis Ababa na atakuwa anasafiri nchi nyingi kutekeleza majukumu yake ya bara. Majukumu haya yanaonekana kama yanayoweza kutatiza wajibu wake wa kisiasa nchini lakini wadadisi wanapinga maoni hayo.

“Bw Odinga angali sehemu kubwa ya siasa za Kenya. Tofauti ni kwamba atakuwa akizicheza kutoka mahali pengine,” alisema mdadisi wa masuala ya siasa Barrack Muluka.

Naye Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri wa siasa, anasema uteuzi huo utamfaa Bw Odinga kwa kumjengea sifa barani na ulimwenguni.

“Ataendelea kucheza siasa humu nchini na kuendeleza azma yake ya kuwa rais na pia kushinikiza kura ya maamuzi kuhusu Katiba,” alisema Prof Munene.

Kulingana na kiranja wa upinzani bungeni Junet Mohammed, kinara wao hataacha siasa mbali ataendelea kusukuma ajenda ya mageuzi.

Kwa miongo mitatu, Bw Odinga amekuwa sura ya upinzani nchini Kenya na kukubali kwake uteuzi wa AU huenda kukazima kabisa upinzani Kenya ambao umefifia tangu alipoafikia muafaka na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi.

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta alikuwa katika msitari wa mbele kushawishi AU kumpatia Bw Odinga wadhifa wa kimataifa.

Akiwa Mjumbe wa AU, Bw Odinga atakuwa amepanda hadhi na hivyo kutokuwa na wakati mwingi wa kuhusika na siasa za humu nchini. Hii huenda ikawa afueni kwa Bw Ruto anayemuona kama mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na pigo kwa upinzani ambao amekuwa nguzo muhimu kwake.

Ikizingatiwa kuwa muafaka wake na Rais Kenyatta ni wa kuunganisha Wakenya, huenda Odinga akaendelea kuvuma katika siasa za humu nchini.

Kiongozi wa wengi katika bunge la Aden Duale ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto anasema Odinga hafai kusahau mchakato wa kuunganisha Wakenya alioanzisha pamoja na Rais Kenyatta.

Akimpongeza Bw Odinga kwa uteuzi wake, Rais Kenyatta alisema utasaidia Kenya kuafikia malengo yake ya ruwaza ya 2030 na kutimiza Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee.